Wafanyabiashara watakiwa kusajili biashara zao kisheria

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 10:59 AM Dec 25 2024
Meneja Kanda ya Mashariki Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Noor Meghji.
Picha:Mtandao
Meneja Kanda ya Mashariki Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Noor Meghji.

WAFANYABIASHARA mkoani Pwani wametakiwa kusajili bidhaa zao na wenye viwanda wahakikishe wanathibitisha ubora kabla ya kwenda sokoni.

Rai hiyo ilitolewa mwishoni mwa wiki na Meneja Kanda ya Mashariki Shirika la Viwango Tanzania (TBS), Noor Meghji, kwenye maonesho ya viwanda na uwekezaji yaliyofanyika mkoani humo.

Aidha, aliwataka wazalishaji wadogo kuthibitisha bidhaa zao, kwa kuwa serikali kupitia TBS inatoa huduma ya bure ya kuthibitisha bidhaa kwa wajasiriamali na kinachotakiwa ni wao kutambuliwa na Shirika la Viwanda Vidogo (SIDO).

"SIDO ni taasisi mama inayohudumia wazalishaji wadogo, basi itakapokutambulisha kwetu huduma ya uthibitishaji wa bidhaa hiyo unakuwa ni bure, kwa hiyo hakuna sababu yoyote ya kupeleka bidhaa sokoni bila kuwa na nembo ya ubora," alisema Meghji.

Alipongeza jitihada ambazo zimefanywa na Mkuu wa Mkoa wa Pwani kufanikisha maonesho hayo na kwamba TBS imeshiriki ili kuwahimiza washiriki wa maonesho hayo kuzingatia ubora wa bidhaa wanazozalisha.

"Iwapo haujathitibisha ubora wa bidhaa unazozalisha, haujathibitisha ubora wa mifumo, basi biashara na uwekezaji huo hauwezi kuwa endelevu," alisema.

Aliwaeleza washiriki wa maonesho hayo majukumu ya shirika hilo na huduma zinazotolewa na TBS.

Meghji alisema majukumu ya TBS ni kuhamasisha masuala ya viwango, kufanya uthibitishaji wa bidhaa pamoja na mifumo, ukeshaji upimaji wa bidhaa husika, kufanya ukaguzi maeneo mbalimbali yanayohusika na uuzaji na usambazaji wa bidhaa.

Alitaja mengine kuwa ni kusimamia bidhaa zinazoingia nchini kuhakikisha ni zile zenye ubora  na salama ndizo zinazoingia nchini kwa kufanya ukaguzi wa bidhaa kabla ya kuingia nchini.

Aidha, Meghji alisema TBS inatoa huduma za kimaabara na lina maabara tisa ambazo zinahusisha upimaji bidhaa mbalimbali.

"Pia tunatoa huduma ya upimaji binafisi kwa wanaohitaji huduma hii, kwa mfano mzalishaji yeyote anayetaka kuuza nje ya nchi kuna huduma TBS tunatoa kuwezesha wazalishaji kusafirisha bidhaa zao kwenda nje,” alisema.

"Unaweza kuwa unataka kupeleka bidhaa nje ya nchi ukaambiwa tunataka bidhaa hiyo iwe imetambuliwa na taasisi kutoka nchi yako ambayo inathibitisha ubora na usalama wa bidhaa hiyo, basi TBS tunatoa huduma hiyo," alisema.