Waziri Bashe aitaka TARI kuongeza tafiti mbegu za asili

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 06:48 PM Oct 01 2024
Waziri Bashe aitaka TARI kuongeza tafiti mbegu za asili
Picha:Mtandao
Waziri Bashe aitaka TARI kuongeza tafiti mbegu za asili

WAZIRI wa Kilimo, Hussein Bashe, ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kuongeza zaidi tafiti na uzalishaji wa mbegu za asili ikiwamo kuwajengea uwezo zaidi watafiti wake kupitia vyuo vya ndani na nje ya nchi.

Bashe ametoa agizo hilo kupitia kwa Mkurugenzi Mkuu wa TARI, Dk. Thomas Bwana wakati wa ziara yake katika Kituo cha Utafiti cha TARI - Naliendele, mkoani Mtwara. 

Katika ziara hiyo, Bashe alikagua  na kupata taarifa kutoka kwa watafiti kuhusu tafiti za mbegu za korosho, ufuta, karanga, njugu na mboga mboga.

“Naelekeza pia nyaraka za kuanzisha mfuko wa kufanya tafiti za kilimo ‘agricultural research fund’ na kanuni zake ziandaliwe ili kuiwezesha TARI kutunza rasilimali fedha zitakazotokana na makato ya mazao kwa lengo la kuwezesha uendelezaji wa tafiti za kilimo nchini,” alisema Bashe. 

Bashe alitolea mfano wa makusanyo yanayotokana na makato kwenye mauzo ya zao la Korosho ambapo kwa Mikoa ya Mtwara na Lindi ni Sh.25 kwa kila kilo; huku zao la ufuta ni likiwa shilingi moja hadi mbili kwa kilo kwa mikoa hiyo. 

 “Mfuko wa ‘Agricultural research fund’ ukishapatikana, tutaweka utaratibu kwa mazao mengine ili makusanyo hayo yaendeshe shughuli mbalimbali kama vile tafiti au kujenga uwezo kwa watafiti,” alisema Bashe. 

Kwa upande wa uzalishaji wa mbegu, Bashe alielekeza wataalamu waanze kuainisha mbegu tofauti kwa kila zao kama vile za asili, za kisasa, organic, hybrid ili hata mkulima akienda dukani awe na nafasi ya kuchagua aina ya mbegu anayoitaka kutoka kwenye aina mbalimbali za mbegu ya zao moja. 

Wataalamu wa TARI - Naliendele walisema wamegundua  aina za mbegu bora 64 za zao la korosho, ambalo linalokabiliwa na visumbufu vya wadudu aina mbalimbali wakiwemo Ubwiriunga, Dieback na Vidung’ata.