CHAMA cha ACT Wazalendo, kimewataka Watanzania kuungana kuilazimisha serikali kutekeleza wajibu wake katika kushughulikia tatizo la ajira nchini na kuhakikisha inaondoa mazingira kandamizi kwa watu wanaofanya biashara binafsi.
Aidha, kimewataka vijana na wazazi kutumia uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2024 na Mkuu ujao 2025 kukiondoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) madarakani kwa kuwa kimeshindwa kutatua tatizo la ajira.
Wito huo ulitolewa leo na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Bara, Isihaka Mchinjita akiwa Mlimba, mkoani Morogoro baada ya kubaini eneo hilo na mengine kuna ongezeko kubwa la vijana wanaohitimu ngazi mbalimbali za elimu na kukosa ajira licha ya taifa kutumia gharama kubwa kuwasomesha.
“Mwaka huu pekee 2024-2025 Fedha zinazotokana na kodi takribani Sh. bilioni 800 zitatumika kusomesha watoto wa vyuo vikuu zinatolewa kama mikopo.
“Kwa wanafunzi ni kodi zenu ambazo zinatozwa kwenye mazao nyingine mnaponunua bidhaa mnakatwa VAT tunafanya haya kila mwaka lakini ajira zinazozalishwa kila mwaka ni chache,” amesema Mchinjita.
Amesema kila mwaka vijana milioni moja wanaingia kwenye soko la ajira, na uwezo wa serikali ya CCM ya kuajiri kwa sasa ni vijana elfu 70 tu kwa mwaka. Na kwamba kila mwaka vijana 930,000 wanarudi mtaani wakiwa hawana ajira, imefikia mahali serikali haijui kesho ya kizazi cha Taifa hili.” amesema Mchinjita.
Akifafanua upungufu wa watumishi amesema sekta ya elimu kuna upungufu wa walimu 279,202 na watumishi wa afya 121, 998. Lakini serikali haijaweka mkazo kuhakikisha sekta hizo zinapata wahudumu na wafanyakazi, licha ya kuwepo kwa vijana waliosomeshwa kwa gharama kubwa, serikali ina waacha mtaani wanakuwa machinga, bodaboda na mamantilie.
Akiwa Wilayani Chato mkoani Geita, Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu, ameitaka serikali ifanye uchunguzi wa kina kuhusu visa vya watoto kupotea na kuuawa vinavyoripotiwa Kanda ya Ziwa.
Ado amesema alipokwenda Busega aliwakuta wananchi wanalia watoto wao wamepotea akisisitiza katika maeneo hayo visa hivyo vinaongezeka.
“Sisi ACT Wazalendo, tumepaza sauti mara nyingi ili Rais Samia Suluhu Hassan kupitia vyombo vyake vya ulinzi na usalama atumie intelejinsia ya serikali kubaini wanaopotea na kuuawa wanakwenda wapi.
“Kule Busega nilikuta kisa cha watu waliovamia kituo cha polisi kwaajili ya matukio ya watoto walio uawa, wito wetu baadala ya kuhangaika na wananchi wenye hasila kali lazima serikali iwajibike kukomesha vitendo hivyo,” alisema Ado huku akishangiliwa na wananchi.
Amesema Rais anapaswa kulitazama jambo hilo kwa uzito mkubwa kwamba anafahamu aliunda tume ya kuchunguza kuuawa kwa mwananchama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Ally Kibao lakini isiwe kwa huyo pekee kwakuwa visa ni vingi.
Aidha, amesisitiza ni vizuri iundwe tume yenye hadhi ya kijaji na sio Jeshi la Polisi lijichunguze lenyewe.
“Kama jambo hilo halitofanyiwa kazi Waziri wa Mambo ya Ndani, Hamad Masauni ajihudhuru sambamba na Mkuu wake wa Jeshi la Polisi (IGP) Camilius Wambura huu ujumbe ninaupeleka kwa Rais kwa sababu ziara ya Katibu Mkuu inafuatilia
“Tukikaa kimya ndugu zangu bila kupigia kelele masuala haya hakuna atakayebaki salama ninaiomba serikali iyafanyie kazi” amesisitiza Ado
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED