PURA, M&P zajadili mradi wa uchorongaji visima vipya vya gesi asilia

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 06:33 PM Oct 01 2024
Wajumbe walioshiriki kakao kati ya PURA na M&P kilichofanyika Septemba 30, 2024 kwa lengo la kujadili mradi wa uchorongaji wa visima vitatu katika Kitalu cha Mnazi Bay.
Picha:Mpigapicha Wetu
Wajumbe walioshiriki kakao kati ya PURA na M&P kilichofanyika Septemba 30, 2024 kwa lengo la kujadili mradi wa uchorongaji wa visima vitatu katika Kitalu cha Mnazi Bay.

MAMLAKA ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imefanya mazungumzo na mwendeshaji wa Kitalu cha Mnazi Bay, Kampuni ya Maurel et Prom Exploration Production Tanzania Ltd, kwa ajili ya kujadili mradi wa uchorongaji wa visima vitatu vipya vya gesi asilia unaotarajiwa kutekelezwa mwanzoni mwa mwaka 2025.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye vyombo vya habari na uongozi wa PURA, Mradi huo unatarajiwa kugharimu Dola za Marekani Milioni 80.2

Uchorongaji wa visima hivyo vitatu vipya utawezesha kuimarisha uzalishaji na upatikanaji wa taarifa za kijiolojia kuhusu mashapo yaliyo katika Kitalu hicho.

Kati ya visima vitakavyochimbwa, viwili vitakuwa vya uzalishaji na kimoja  kitakuwa cha utafutaji. 

Taarifa hiyo ya PURA ilieleza kuwa kitalu cha Mnazi Bay tayari kina visima vitano vinavyozalisha gesi asilia kwa wastani wa futi za ujazo milioni 74.24 kwa siku.

Wabia katika Kitalu hicho kilichopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara ni M&P ambaye ni mwendeshaji mwenye ushiriki wa asilimia 60 katika shughuli za uzalishaji na TPDC mwenye asilimia 40.

"Kuelekea utekelezaji wa mradi, tathmini ya athari kwa mazingira imekamilika na utaratibu wa fidia kwa wananchi watakaopisha mradi linatarajiwa kuanza mapema mara baada ya uhakiki kukamilika,"ilieleza.

"PURA na M&P zilijadilia pia ushiriki wa watanzania na watoa huduma wa kitanzania katika zabuni zinazotokana na mradi huo na katika eneo hili, Mamlaka imemtaka mbia kuhakikisha anazingatia matakwa ya sheria kuhusu ushiriki wa watanzania."

Pia, mamlaka hiyo ilieleza kuwa inafuatilia kwa karibu kila hatua ya utekelezaji wa mradi huo kuhakikisha Watanzania na watoa huduma wa Kitanzania wanashiriki kikamilifu.