Viongozi watoto waanza kushirikishwa kuukabili ukatili wa kijinsia mtaani

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 07:22 PM Oct 01 2024
Watoto wakiwa katika uchaguzi wa viongozi wa kamati za kuwasikiliza mitaani.
PICHA: SABATO KASIKA
Watoto wakiwa katika uchaguzi wa viongozi wa kamati za kuwasikiliza mitaani.

UKATILI wa kijinsia dhidi ya watoto, wasichana na wanawake, ni miongoni mwa matukio yanayoleta fedheha katika familia na taifa pia.

Watoto wananajisiwa, kuteswa, kupata vipigo kupindukia, kutakanwa na kunyimwa mahitaji muhimu. Na wakati wote wanaowafanyia hayo wanawaambia usimwambie mtu, ukisema nitakumaliza. 

Katika juhudi za kukabiliana na ukatili  kama huo, wadau wa kutetea haki za wanawake na watoto  wameunda kamati za uongozi zinazoongozwa na kusimamiwa na watoto kukabiliana na migogoro na ukatili dhidi yao.

 Kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni jijini Dar es Salaam kinachojihusisha na vita dhidi ya ukatili wa kijinsia ukiwamo ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni na rushwa ya ngono kimeunda kamati hizo za kiuongozi ili watoto washiriki kupiga vita. 

Mwenyekiti wa kituo hicho Fatma Twalib, anaiambia Nipashe kwenye mahojiano hivi karibuni kuwa, wameunda kamati za uongozi wa watoto mtaani baada ya kubaini kuwapo kwa ukatili unaofanywa na jamaa wa karibu na wazazi kuanzia baba, mjomba, shangazi na ndugu wengine ndani ya familia lakini unafichwa. 

"Tunaamini watoto hao watashirikishana kusikiliza na kufuatilia ukatili unaowakabili, kuamua migogoro yao midogo midogo na kupeleka kwenye uongozi mambo mazito,” anasema. 

Anaeleza kuwa iwapo watu wazima wana utaratibu na uongozi wao, hata watoto wanahitaji kuwa nao, hivyo wameamua kuwaandaa na kuuanzisha. 

 Anaeleza kuwa kupitia uongozi wa watoto, anaamini kuwa watakuwa wamepanua wigo kwa watoto hao kuripoti matukio ya ukatili ambayo yamekuwa wakitokea kwenye jamii.

 "Tuliamua kuwakusanya katika maeneo yao wanayochezea ya kuwapa wazo hilo, wakubali na tukawapa nafasi ya kuchagua uongozi wao, wakachaguana, hivyo sasa wana uongozi wao," anasema.

 Mwenyekiti huyo anafafanua kuwa, katika harakati ambazo kituo hicho kimekuwa kikifanya, wamebaini kuwa kuna mambo ambayo mtoto hawezi kumwambia mama au baba, bali rafiki yake wa karibu.

 "Lakini hata rafiki yake akiambiwa, hajui ataitatuwaje changamoto hiyo, lakini kupitia uongozi tulioutengeneza, mtoto akiwa na tatizo atapeleka kwa kiongozi wao, naye atatuletea sisi,  tumewapa mafunzo ya jinsi ya kutatua migogoro midogo," anasema.

 Katika utatuzi huo wa migogoro  midogo, Fatma anasema watoto hao wataanza kwa kesi ndogo ndogo zikiwamo za kuibiana kalamu, kutoleana matusi na kupigana.

 Anasema wakifanikiwa kutatua migogoro hiyo midogo, ni wazi huo utakuwa ni mwendelezo wa mafanikio ya kufikia lengo la kituo hicho la kushirikisha watoto kutoa taarifa za matukio ya vitendo vya ukatili na ndani ya jamii vinavyoumiza watoto, wasichana na wanawake.

 "Kituo cha Sauti ya Jamii tumekuja na ubunifu huu, tunatamani kuona ukiigwa nchi nzima, kwa sababu vitendo vya ukatili vimeenea kote, si hapa kwetu tu," anasema.

 Anaeleza  ni lazima kuchukua hatua za kuwalinda na kuwaepusha waathirika hao na ukatili lakini pia na kuwadhibiti watuhumiwa.

 Anasema kwa sasa kituo kimeona ni lazima kila mmoja ashiriki kuanzia watoto ndiyo maana kituo hicho kimekuja na mbinu mpya ya kuwahusisha watoto katika vita hiyo, kwa kuunda uongozi wa watoto mtaani ili waweze kueleza katika uongozi wao madhila wanayokumbana nayo.

Anafafanua kuwa wameunda kamati tatu za ukatili, elimu na mazingira na kwamba wanafunzi uongozi wao, wamo wa darasa la pili hadi hadi la  sita.

"Bado tunaendelea kupanga ratiba yao ya jinsi ya kututana kila mwishoni mwa wiki na kuweka yao ya kupambana na ukatili ndani ya familia na ndani ya jamii.

 SAUTI ZA WATOTO

 Mwenyekiti wa uongozi wa watoto hao Yasinta Mpoze, anasema anaamini nafasi aliyoipata ni mwanzo mzuri kwake wa kujiandaa kuwa kiongozi wa baadaye, kwa kuwa anapata uzoefu kupitia jukumu hilo.

 "Walichokifanya Kituo cha Sauti ya Jamii, ni jambo jema kwetu watoto, kwani mbali na majukumu mengine tulionayo, ni kama kutuandaa kuwa viongozi wa baadaye kupitia uzoefu na mafunzo tunavyopitia," anasema Yasinta.

 Anasema watoto wana mambo mengi wanayokumbana nayo yakiwamo ya kuonewa na wenzao ambao ni wababe, huku wakiogopa kuwataja na kwamba kupitia uongozi huo watawaelekeza jinsi ya kuwa huru.

Yasinta anasema yapo mafunzo ya uongozi wanayopata kituoni ambayo watayatumia kusaidia wenzao kubadili tabia na wengine na kuachana na mienendo ya uhalifu na uchokozi.

"Lakini pia tutasaidiana na kuelekezana kuacha  au kuficha ukatili, badala yake watuambie ili na sisi tuyafikishe katika kituo cha Sauti ya Jamii Kipunguni kwa hatua zaidi," anasema.

 Katibu wa uongozi wa watoto hao Stan Mhagama, anakishukuru kituo hicho kwa kuwashirikisha katika mambo makubwa ambayo jamii na AZAKI nyingi hazijafikiria umuhimu wa kutumia watoto kutatua migogoro ya namna hiyo.

 Mhagama anasema yeye na viongozi wenzake watajitahidi kufanya kile ambacho wataweza ili kusaidia katika vita dhidi ya ukatili wa watoto kwa kuwa karibu na viongozi wa kituo hicho kupata uzoefu.

 "Tutaongoza watoto wenzetu kadri inavyowezekana ili kusaidia watoto wenzetu kufunguka wanapofanyiwa ukatili na wazazi wao, ndugu zao au watoto wenzao ama wanafunzi wenzao," anasema Mhagama.

 Mmoja wa wazazi wa watoto hao, Oresta Mhagama anasema ushirikishwaji wa watoto unaotakiwa katika kipindi hiki ambacho dunia imeharibika na kusababisha kuwapo kwa matukio ya kutisha.

 "Kuna ripoti  mtoto ameharibiwa kwa kulawitiwa au kufanyia kitendo chochote cha ukatili, hasemi, lakini kupitia uongozi wao, tunaamini wale wote waliokumbana na madhila hayo wanaweza kufikisha taarifa kwa wenzao ili wayafikishe katika kituo hicho," anasema Oresta.

 Oresta anaongeza: “Kuanzisha uongozi wa watoto ni hatua mojawapo ya ushirikishaji wa watoto katika vita dhidi ya ukatili ambao umeleta madhara na vifo kwa baadhi yao katika maeneo mbalimbali.”