Ujasusi teknolojia ya kielektroniki ulivyoangamiza mkuu wa Hezbollah

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:19 PM Oct 01 2024
Hassan Nasrallah, aliyeuawa na  Jeshi la Israel.
PICHA: REUTERS
Hassan Nasrallah, aliyeuawa na Jeshi la Israel.

KIKUNDI cha Hezbollah cha Lebanon kimeumia kwa mambo mengi wiki iliyopita ikiwa ni pamoja na kumpoteza kiongozi wake Hassan Nasrallah.

Hasara nyingine imetokana na kuharibiwa vifaa vyake vya  mawasiliano na simu za upepo zinazotumiwa na Hezbollah.  

Kwa miaka 32 iliyopita, Hezbollah haijamjua kiongozi na katibu mkuu isipokuwa Hassan Nasrallah, ambaye aliuawa Ijumaa iliyopita katika mashambulizi ya Israel yaliyolenga makao makuu ya chama hicho kusini mwa mji mkuu wa Lebanon Beirut.

Israel ilifanya mashambulizi ya anga katika mji mkuu wa Lebanon Beirut Ijumaa iliyopita na kumuua Nasrallah. 

Kabla ya hapo kulikuwa na milipuko kadhaa mwezi uliopita ulijeruhi zaidi ya wapiganaji 1,500, huku wengine kadhaa wakipoteza maisha.

Swali linaloulizwa ni kwa namna gani vikosi vya usalama vya Israel vilimsaka Nasrallah na kufanikiwa kuwalenga makamanda wakuu wa Hezbollah?

Kwa mujibu wa mwandishi wa usalama wa BBC, Frank Gardner, kumlenga Nasrallah ulikuwa uamuzi wa kimkakati wa Israel.

Anasema kwa miaka kadhaa iliyopita walikuwa wakiishi mafichoni na Israel ilikuwa ikiwafuatilia.

"Maelfu ya vifaa vya mawasiliano vya Hezbollah na simu za upepo vililipuliwa hivi karibuni. Inaaminika kuwa shirika la kijasusi la Israel linahusika."

"Kutokana na kila kitu kilichotokea tangu wakati huo, ni wazi kuwa Israel imejikita sana katika muundo wa Hezbollah." Anasema.

Anaongeza kuwa wakati jeshi la Israel linasema limewaondoa makamanda wakuu wote wa Hezbollah, swali ni jinsi lilivyovizuia kwa ufanisi vyombo vya usalama vya Hezbollah.

KUPATIKANA NASRALLAH 

Kwa mujibu wa ripoti maalum ya shirika la habari la Reuters, Nasrallah alizungumza na vyanzo kadhaa vya Lebanon, Iran na Syria kabla ya kifo chake.

Shirika la habari la Reuters, likinukuu chanzo, kimoja linadai kuwa Israel ilikuwa ikifanya ujasusi dhidi ya Nasrallah na Hezbollah kwa miaka 20 kabla ya kushambulia makao yao makuu.

Maofisa wawili wa Israel wanaiambia Reuters kwamba Waziri Mkuu Benjamin Netanyahu na kamati maalumu ya mawaziri waliidhinisha shambulio hilo  Jumatano iliyopita.

Ni wakati huo huo, Netanyahu alikuwa akihutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mjini New York, Marekani.

Matthew Saville ni Mkurugenzi wa Huduma za Kijeshi katika Taasisi ya Royal United Services, anayesema inaonekana kuwa mpango huo umekuwa ukifanya kazi kwa miaka mingi na unaweza kuwa umetekelezwa katika viwango kadhaa.

"Inaonekana kulikuwa na utekaji nyara wa mawasiliano, pia kusikiliza maagizo ya siri au mazungumzo au kupata habari kuhusu wahusika.

Aidha, huenda pia kulikuwa na 'uchambuzi wa picha' za satelaiti au picha zilizopigwa kwa siri ambayo ni pamoja na  kupata taarifa za siri zinazotolewa na wanadamu.

Kwa maneno mengine, wapelelezi walio chini wanaweza kuwa na jukumu kubwa pia la kufuatilia na kusaka habari hizo.

Baada ya vita vya 2006 kati ya Israel na Hezbollah, Nasrallah aliacha kusafiri hadharani tena asiyeonekana kwa wepesi.

Chanzo kilicho karibu na usalama wa Nasrallah kinaliambia shirika la Reuters kwamba kiongozi huyo yuko katika hali ya tahadhari. 

Anaelezwa kuweka vikwazo vikubwa na alikuwa akikukutana na watu wachache sana.

Maofisa watatu waandamizi wa jeshi la Israel wanaliambia gazeti la Marekani la 'The New York Times' Jumamosi iliyopita  kwamba walikuwa na taarifa kuhusu mahali alipo Hassan Nasrallah kwa miezi kadhaa.

Kwa mujibu wa ripoti za Israel, uamuzi wa kumlenga Nasrallah ulifanywa mara moja na bila ya kuifahamisha Marekani, ili wasipoteze muda.

Kwa mujibu wa ripoti ya Reuters, Nasrallah alikuwa katika hali ya tahadhari baada ya milipuko ya vifaa vya mawasiliano, kwani haikuwa siri kuwa Israel ilitaka kumuua.

Hakujumuishwa hata katika msafara wa mazishi ya makamanda wa Hezbollah, na hotuba zake zilizorekodiwa kabla kusikilizwa siku chache baadaye.

Israel inasema makao makuu ya Hezbollah yalikuwa chini ya jengo la makazi ya watu kusini mwa Beirut, ambapo bomu lilimlenga Nasrallah.

Jeshi la Israel linasema kuwa limewaua makamanda tisa wa jeshi la Hezbollah akiwamo Nasrallah katika muda wa wiki moja.

Magnus Ranstort wa Chuo Kikuu cha Ulinzi cha Uswizi ni mtaalam anayefuatilia masuala ya Hezbollah.

Anasema  maendeleo haya ni kikwazo kikubwa kwa Hezbollah, ambayo inafichua kushindwa kwa intelijensia yake.

Magnus anasema:"Wao- Waisraeli walijua kwamba Nasrallah alikuwa akifanya mikutano, akikutana na makamanda wengine aliposhambuliwa."

Akizungumza na waandishi wa habari  Jumamosi, msemaji wa jeshi la Israel Luteni Kanali Nadav Sheshani, anasema kuwa alikuwa na taarifa za 'muda halisi' kuhusu mkutano kati ya Nasrallah na viongozi wengine.

Hata hivyo, Seshani hakufafanua jinsi taarifa hizo zilivyokuwa zikipatikana akisema wanakwenda kukutana ili kushambulia Israel.

Brigedia Jenerali Amichai Levin, Kamanda wa Jeshi la Anga la Hatjerim la Israel, anawaambia waandishi wa habari kwamba makumi ya mabomu yalirushwa ndani ya sekunde.

"Hii ilikuwa operesheni ngumu sana na ilikuwa imepangwa kwa muda mrefu," anasema.

Kwa mujibu wa Saville, ndege za kivita za Jeshi la Anga la Israel F-15 zimeripotiwa kudondosha mabomu takribani 80, yenye uwezo wa kuharibu ngome hiyo, baada ya kupata taarifa halisi kuhusu eneo la Nasrallah."

Taarifa zinasema mabomu yalirushwa yakilenga vyumba vya chini ya ardhi huko Beirut Kusini na Dahiya. Hapa ndipo Nasrallah alipokuwa akikutana na makamanda wengine.

Na kwamba kutokana na hayo yote ni wazi kwamba mashirika ya kijasusi ya Israel yalifanikiwa kupenya vyombo vya usalama vya Hezbollah.

Nafasi ya Nasrallah hivi karibuni itachukuliwa na mtu mwenye sifa zinazofanana na hizo za kidini. Lakini itamchukua miaka kiongozi huyo mpya kupata wafuasi.