Samia ahimiza viongozi uaminifu, nidhamu

By Jenifer Gilla , Nipashe
Published at 10:54 AM Oct 01 2024
Rais Samia Suluhu Hassan akibonyeza kitufe kuashiria uzinduzi wa kitabu kuhusu Maisha na Uongozi wa Hayati Edward Moringe Sokoine, aliyekuwa Waziri Mkuu mwaka 1977 mpaka 1980 na 1983 hadi 1984, katika hafla iliyofanyika jijini Dar es Salaam jana.

RAIS Samia Suluhu Hassan amewakumbusha viongozi kuiga mfano wa aliyekuwa Waziri Mkuu, Hayati Edward Sokoine, kwa kufanya kazi kwa uaminifu, nidhamu na uchapakazi. Amesema wakifanya hivyo vyeo vitawafuata badala ya kuvikimbilia.

Aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam katika hafla ya uzinduzi wa kitabu cha kiongozi huyo cha ‘Edward Moringe Sokoine, Maisha na Uongozi Wake’.

Rais Samia alisema viongozi wakifanya kazi kwa bidii na uaminifu, hawatokuwa na haja ya kukimbizana na vyeo bali vitawafuata kulingana na matokeo ya utendaji kazi wao.

“Katika hili tunajifunza kwamba ukiwa mwadilifu na mchapakazi, huna haja ya kukimbizana na vyeo bali vyeo vitakufuata ulipo,” alisema.

Alisema Sokoine alikuwa mwaminifu kwa mamlaka yake ya uteuzi na wananchi ndiyo maana alipewa majukumu mengi katika umri mdogo, ikiwamo uwaziri mkuu.

Rais alisema kitabu hicho pia kinawafundisha yeye (Samia) na viongozi vijana kufanya mambo yatakayoacha alama kwa kuwa kiongozi huyo aliacha alama katika kila ngazi aliyoifanyia kazi kwa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo ikiwamo ujenzi wa reli wa TAZARA.

Alisema alama nyingine aliyoiacha ni alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kushauri na ikapitishwa kuwa wanawake waandikishwe jeshini na mpaka sasa kuna viongozi wa nafasi za juu katika jeshi hilo.

MAGEUZI YA KILIMO

Pia alisema Sokoine aliamini katika kilimo cha kisasa kupitia wataalamu, hivyo alisimamia uanzishwaji wa Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) ambacho mpaka sasa kinaishi maono yake ya kuzalisha wataalamu wengi wanaoendeleza sekta za kilimo na mifugo.

Alisema tangu kufariki dunia kiongozi huyo, serikali imeendelea kutoa kipaumbele kwenye sekta ya kilimo kwa kuongeza bajeti kila mwaka hadi  kufikia Sh. trilioni 1.25 kwa mwaka wa fedha 2024/25, iliyosaidia kuongeza maofisa ugani na kuwapatia vitendea kazi.

Ongezeko la bajeti, pia alisema limesaidia kuzalisha mbegu bora nchini, kutoa ruzuku kwa wakulima na kuongeza eneo la umwagiliaji hali iliyoongeza utoshelevu wa chakula hadi asilimia 128.

Alisema Sokoine alitaka viongozi wote wawe na mwelekeo mmoja na nia ya kulivusha taifa linapopitia wakati mgumu na kujiepusha kuanzisha sababu na vikwazo vya maendeleo bali wajikite kutafuta ufumbuzi wa matatizo.

Rais alisema kauli hiyo inaakisi mapito ya nchi hiyo katika vipindi mbalimbali kama vile mafuriko, hali ngumu ya uchumi, maradhi, vita na katika yote hayo viongozi wa nchi walitembea na maelekezo ya kiongozi huyo na hawakurudi nyuma hali inayosababisha uchumi kuwa himilivu.

“Nasema haya ili kuweka msisitizo kwetu kama viongozi kutokukwamishwa na changamoto zinazotukabili katika vipindi vigumu bali kutafuta njia mwafaka za kujikwamua na tuweze kusonga mbele,” alisema.

Alisema kupitia kitabu hicho, nchi itajifunza ushahidi na maelezo mapya kuhusu mapito ya taifa ambapo serikali inapata uelewa wa kufanya uamuzi kulingana na hali ilivyo sasa.

Rais alisema kitabu hicho kinafundisha kuwa kiongozi si sababu ya kuacha malezi ya watoto kwa kuwa katika uongozi wake, Sokoine alikuwa baba na mlezi aliyesimamia nidhamu kwa watoto wake.

Alisema kiongozi huyo alisimama imara nchi ilipokumbwa na changamoto za kiuchumi, viwanda na afya na uhaba wa chakula, akiweka mkazo kuendeleza kilimo na kuruhusu biashara huria ili kukidhi mahitaji ya wananchi na kuboresha huduma.

Awali, Makamu wa Rais, Dk. Phillip Mpango alimshukuru Rais Samia kwa kuridhia kuandikwa kwa tawasifu ya kiongozi huyo, kuidhinisha Sh. milioni 200 kwa ajili ya kukamilisha shughuli hiyo pamoja na kuandika dibaji ya kitabu hicho.

Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Paramagamba Kabudi, alisema kitabu hicho kinaelezea alama alizoziacha kiongozi huyo katika uongozi ikiwamo kuleta mapinduzi ya kilimo, kupambana na wahujumu uchumi, mageuzi ya elimu na utawala bora.

Alisema katika sura ya nne ya kitabu hicho inaeleza alivyopigania uwapo wa ofisi za bunge katika majimbo ambapo baada ya kula kiapo cha kuwa Mbunge wa Jimbo la Masai mwaka 1965 alihoji bunge ni lini ofisi za bunge zitajenga katika wilaya ambazo hazikupata ofisi ikiwamo ya Monduli.

“Katika nafasi hiyo ya ubunge wananchi wa Jimbo la Masai walimwona kuwa kiuongozi mwaminifu, mwadilifu, mkweli, asiyemlanguzi wa siasa,” alisema.

Prof. Kabudi alisema kitabu hicho kinaelekezea mambo makubwa aliyoyafanya kiongozi huyo katika vipindi viwili walivyohudumu kama waziri mkuu ikiwamo kufanya kazi katika mazingira magumu.

Pia alisema Sokoine alikuwa mwanasiasa makini na mahiri aliyetetea kwa nguvu zake zote watu aliowaongoza hasa wanyonge, alikuwa mkweli na hakuogopa kusema na kutenda aliyoyaamini, alichukia uvivu na ubabaishaji katika maisha, hivyo alisimamia utekelezaji wa sheria, kupiga vita ubadhirifu wa mali za umma, wizi na uzembe.