DALILI za tatizo la akili miongoni mwa wanajamii, hasa mahali pa kazi zinaweza kutambulika kirahisi, hivyo hatua kuchukuliwa haraka ili kumsaidia mwathirika na kumlinda dhidi ya vitendo hasi ikiwamo kujitoa uhai.
Aidha, imeelezwa kuwa afya ya akili ni ustawi kijamii, hivyo kuna umuhimu wa kuwapo utulivu wa kiakili mahali pa kazi na kupewa kipaumbele katika utoaji elimu namna ya kukabiliana na tatizo hilo.
Muuguzi Mtaalamu wa Afya ya Akili kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Sofia Sanga, aliyasema hayo jana katika mada iliyohusu Umuhimu wa Kujali Afya ya Akili Mahali pa Kazi, kupitia mtandao iliyoandaliwa mwishoni mwa wiki na Hospitali ya Taifa ya Afya ya Akili Mirembe (MNMH).
Kadhalika, alisema mahali pa kazi hutumia zaidi ya asilimia 50 ya saa 24 kwa siku, katika kazi rasmi au isiyo rasmi yenye lengo la kujipatia kipato, hivyo ni miongoni mwa maeneo ya chanzo cha ustawi duni wa akili, kutokana na ukosefu wa mbinu za kuzikabili.
Alisema kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), tafsiri ya afya akili imegawanyika sehemu tatu ambazo ni ustawi wa akili; uwezo wa akili binafsi wa binadamu kukabiliana na changamoto mbalimbali maishani; uwezo wa mtu kufanya kazi na kuzalisha; na uwezo wa mtu na mchango wake kwa jamii.
“Tunapozungumzia afya ya akili yaani ustawi wake ni mambo ya kawaida kabisa ambayo yako kwenye jamii. Kwa mfano ya kwanza ni changamoto ambazo ziko zaidi ya madeni mtu anadaiwa. Hii inatosha kabisa kumwathiri mtu asipojua namna ya kukabiliana nayo. Nataja madeni kwa sababu ni suala mtambuka.
“Aidha, deni la benki au mtu binafsi, au dukani kwa Mangi, unadaiwa mikopo ya Vicoba au rafiki yako hata kuna wengine walikula michango ya harusi ikageuka kuwa madeni. Huu ni mfano wa mtu ambaye ukahisi anapitia changamoto,” alisema Sanga.
Aliiitaja changamoto ya pili kuwa ni kama vile kupoteza uhusiano, kazi, kuondokewa na mwenza, ndugu au jamaa. Alisema changamoto hizo zinaweza kupunguza uwezo wa afya ya akili ya mtu yeyote iwapo ustawi wake kiakili utayumbishwa.
Pia alisema viwango vya uwezo wa mtu kwa tafsiri ya pili ni jamii inavyompima katika ufanyaji kazi kama vile kuripoti kazini kwa muda uliopangwa, kutekeleza majukumu na kutoa matarajio kwa asilimia iliyowekwa.
“Mfano kazini mtu ambaye alitarajiwa afanye kitu hiki kulingana na majukumu yake na akaanza kufanya vitu vingine, ujue kuna kitu hakiko sawa kwenye afya yake kiakili. Inawezekana mtu huyu akaingia kazini ndani ya muda asubuhi, lakini anaanza kuzunguka meza moja hadi nyingine na kusimulia watu mambo yake ya nyumbani.
“Labda kuhusu sherehe ya jana au alikuwa klabu au kwenye biashara gani? Mambo ambayo hayahusiani na kazi, hizo ni dalili za kueleza huyu mtu anapitia hali gani katika afya ya akili mahali pa kazi,” alisema.
Kuhusu changamoto kiakili aina ya tatu, muuguzi huyo alisema ni namna mtu alivyo na uhusiano kijamii kuanzia nyumbani, sehemu za ibada, mitaani na hata ofisini.
“Ninaposema jamii ninamaanisha ni zile sehemu zote ambazo tunaishi na jamii. Kila mtu anaishi na watu hatuishi mawinguni. Hata wafanyakazi wenzako wanaweza kukuangalia na kuhisi afya ya akili ina changamoto katika maeneo hayo matatu,” alisema.
”Hii ni namna ambavyo mtu anaweza kuzikabili changamoto kijamii, kuhusiana na jamii inayomzunguka, mahala pa kazi papewe kipaumbele kuliko sehemu zingine, ingawa sehemu zote hata barabarani unapotembea, ili akili isichanganyikiwe usipate shida yoyote,” aliongeza.
Kwa mujibu wa mtaalamu huyo, mahali pa kazi ni eneo ambalo mtu hutumia muda mwingi kufanya kazi wakati mwingine saa 10 10 kati ya 24 za siku, hivyo pakitumika vizuri ni sehemu inayoweza kumtambulisha akili yake kiafya ilivyo, hasi au chanya.
“Mahali pa kazi ndiko mtu anatumia saa nyingi zaidi kuanzia nane hadi 12, ikawa ndio eneo ambalo linatumia saa nyingi zaidi. Lakini saa zilizosalia kati ya 24 matumizi yake yamegawanyika.
“Kuna kulala, kula, kuongea na familia au marafiki, mtu hutumia muda barabarani. Utakuta katika kila tukio anatumia saa mbili au nne, ila kazini ni muda halisi zaidi ya saa nane na kuendelea,” alisema.
Alisema mahali pa kujitafutia riziki ambako hutumia saa nyingi, jamii inayomzunguka mhusika ni rahisi kufahamika tabia zake, kama vile kuomba mapumziko yeye binafsi, akiitaja ni dalili na ustawi duni wa akili.
“Mwingine akifika sehemu ya kazi anakutana na kazi nyingi, hivyo anaamua kulala. Haishiwi sababu nahiyo ni dalili za tatizo la akili. Mtu anajipima binafsi leo ngoja niombe ruhusa nikapumzike ni nzuri, ujue ni dalili ya akili yako inataka kutulia, kuna tatizo,” alisema.
Alitoa wito kwamba mahali pa kazi ili kuepuka ustawi duni wa kiakili, kuna haja ya mtu binafsi kupima matarajio yake na kulinda afya ya akili, huku jamii ikitoa msaada kwa wanaopitia changamoto kiakili kama vile msongo wa mawazo.
“Ukiona mtu awali hakuwa hivi na umemzoa kazini alikuwa hajipambi sana, au kaanza kuvaa mavazi ambayo hayakuzoeleka yanayowaka sana rangi zake, hapo unaweza kuweka kiulizo kwa mwenzako.
“Ukiweza uanze naye taratibu ukibaini kuna tatizo kiakili tulizoea mtu anajipamba kidogo anaanza kujiremba hadi katika macho, anavaa viatu vya rangi za kuwaka, tuzungumze nao kwa upendo,” alisema.
Aliongeza kuwa :“Utakuta mtu ana hisia kali labda katika michezo timu hii imefungwa hatimaye anagombana na wenziie kwa utani, au analia kirahisi, nalalamika kuumwa hapoa na pale, mtu akiingia kazini, anasema amechoka ni dalili za msongo wa mawazo ambazo ni za awali katika tatizo la akili. Au mtu anahisi harufu, sehemu hii inanuka, wengine hawahisi.”
Alisisitiza jamii kufanya mazoezi baada ya kazi ili kuipa akili mawazo mapya na kuipumzisha, kula mlo wenye lishe unaozingatia mahitaji ya mwili, kwa kuwa mlo unaokwenda kinyume huchangia msongo wa mawazo.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED