Polisi Arusha kuchunguza tukio la kifo cha mtu mmoja eneo la Moivaro

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:21 PM Oct 01 2024
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo
Picha:Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo

Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linafanya uchunguzi wa kifo cha mtu aitwaye David Mollel mwenye umri unaokadiriwa kuwa kati ya miaka 50 hadi 55 mkazi wa Baraa Jijini Arusha aliyekutwa amefariki dunia, huku mwili wake ukiwa umening’inia juu ya mti msituni katika eneo la mlima wa Oldonyomasi uliopo kata ya Moivaro Jijini Arusha leo Oktoba 01, 2024.

Akitoa taarifa hiyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Justine Masejo amesema uchunguzi zaidi unafanyika kwa kushirikisha taasisi nyingine za kiuchunguzi kutokana na ujumbe wenye utata uliotumwa kwa ndugu zake watatu jana Septemba 30, 2024 kabla ya kugundulika kwa mwili wake katika mlima huo ukiwa umening’inia.

Aidha mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Arusha kwa ajili ya uchunguzi zaidi.

SACP Masejo amesema kuwa Jeshi la Polisi mkoani humo linatoa  wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na jeshi hilo kutoa taarifa za uhalifu na wahalifu.