Dk. Tulia ahamasisha matumizi Nishati safi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 04:22 PM Oct 01 2024
Spika wa Bunge Tulia Aksoni akimkabidhi jiko la gesi mmoja wa Mama lishe.
Picha: Mpigapicha Wetu
Spika wa Bunge Tulia Aksoni akimkabidhi jiko la gesi mmoja wa Mama lishe.

SPIKA wa Bunge na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini Dk.Tulia Ackson amehamasisha Mama lishe na wananchi kutumia Nishati safi ya gesi ili kutunza mazingira na kuokoa muda wa shughuli za kiuchumi huku akisisitiza kuwa umefika wakati wa kuachana na matumizi ya kuni na mkaa.

Dk.Tulia ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) amesema hayo  leo  jijini Mbeya akiwa na wadau wa Nishati safi ya kupikia kutoka Kampuni ya Gesi ya Oryx na kutembelea Mama lishe kwa lengo la kuwahamasisha kuacha na matumizi ya nishati chafu.

Amesema  lengo ni kuhamasisha watanzania kupikia nishati safi ikiwa ni kuunga mkono kampeni ya Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha wananchi wanatumia Nishati safi badala ya mkaa na kuni.

Meneja wa Miradi ya Nishati Safi ya kupikia kutoka Kampuni ya Gesi ya Oryx, Peter Ndomba, amesema wamekuwa wakisaidia makundi mbalimbali yakiwemo ya Mama na Baba Lishe kupata Nishati safi ya kupikia na kwamba hadi sasa wameshatoa mitungi ya gesi na majiko yake zaidi ya 70,000.

"Oryx tunafahamu dhamira ya Rais Samia Suluhu ni kuhakikisha katika kipindi cha miaka 10 asilimia 80 ya Watanzania iwe inatumia nishati safi ya kupikia na Kampuni yetu imeibeba ajenda hiyo kwa vitendo.

"Leo hii tupo hapa tumeungana na Spika Dk.Tulia ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Mbeya kupitia taasisi ya Tulia Trust tumekuwa naye katika jitihada hizi za Nishati safi. Pia amekuwa mfano na kielelezo cha matumizi ya nishati safi kwa wananchi," amesema.

Ameongeza kuwa kupata kiongozi ambae ameamua kuwa mfano wa moja kwa moja kwa kupika na gesi, kwao imeacha alama kubwa na wamefurahishwa kwakuwa inaongeza chachu katika hamasa ya kusisitiza matumizi ya nishati safi.

"Watu wengi watabadilika, kwani tunafahamu makundi mbalimbali yakiwemo ya Baba na Mama Lishe ambao tunaona kila siku wako katika kuni na mkaa maisha yao yako hatarini.

"Tunaambiwa makundi yanayofanya shughuli za kupika yako hatarini zaidi. Watanzania zaidi ya 33000 wanafariki kila siku kwasababu ya kutumia kuni na mkaa," amesema.

Aidha, amesema Mama na Baba Lishe maisha yao ni moto na kuni hivyo wakianza na kundi hilo wanaweza kuokoa Watanzania.

"Tunashukuru kwa Tulia Trust pamoja na vyombo vya habari kwa kupeleka taarifa kwa umma ili kila mmoja aifuate. Ndani ya wiki tatu zilizopita hapa Mbeya tumetoa mitungi ya gesi 1000 kwa mama na Baba Lishe," amesema.

Spika wa Bunge Tulia Aksoni akifurahia jambo na watoto.