Watu zaidi ya 500 kushiriki wiki ya AZAKi Arusha

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 08:49 AM Aug 27 2024
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge, akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) jijini Dar es Salaam kuhusu wiki ya AZAKi inayotarajiwa kufanyia kuanzia Septemba 9 mpaka 13 mwaka huu
Picha: Elizabeth Zaya
Mkurugenzi Mtendaji wa FCS, Justice Rutenge, akizungumza na waandishi wa habari(hawapo pichani) jijini Dar es Salaam kuhusu wiki ya AZAKi inayotarajiwa kufanyia kuanzia Septemba 9 mpaka 13 mwaka huu

UCHAGUZI wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu mwaka kesho na maandalizi ya Dira ya Taifa ya Maendeleo, zinatarajiwa kuwa miongoni mwa agenda kubwa katika mijadala kwenye wiki Asasi za Kiraia(AZAKi) inayotarajiwa kuanza Septemba 9 mpaka 13 mwaka huu.

Wiki hiyo ya AZAKi inatarajiwa kufanyika jijini Arusha na kushirikisha zaidi ya wadau 500 kutoa katika asasi hizo, sekta binafsi, serikali na wadau mbalimbali wa maendeleo.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jana Dar es Salaam, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Foundation for Civil Society (FCS), Justice Rutenge, alisema wiki hiyo imebebwa na kaulimbiu isemayo 'Sauti, Dira na Thamani'.

Alisema kauli mbiu hiyo inaendana na wakati uliopo na matukio yanayoendelea nchini ambayo ni pamoja na uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka huu, uchaguzi mkuu wa mwakani na uandaaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2025-2050.

"Tupo kwenye kipindi muhimu sana kwenye demokrasia yetu kama nchi, kwa sababu mwaka huu tuna uchaguzi wa serikali za mtaa, wote mnafahamu, pia mwakani tuna uchaguzi mkuu, lakini la jambo la kipekee sana, mwakani tunatarajia kuzindua Dira ya Taifa ya Maendeleo ya  2050 ambayo ni fursa adimu sana inayokuja mara moja kwa muda mrefu. 

"Fursa hii kutokana na umuhimu wake hatuna budi sauti za wananchi zikasikika kuchangia maoni yao wenyewe, kwani Dira ya Taifa inapaswa itokane na sauti, mawazo, mitazamo na maoni ya wananchi," alisema Rutenge.

Rutenge alisema kuwa, wiki hiyo pia itakuwa na mijadala mbalimbali inayohusu shughuli za AZAKi nchini, maendeleo ya jamii na ushirikiano baina ya asasi za kiraia, serikali na sekta binafsi.

Mkurugenzi mkazi wa Shirika la kimataifa linaloshughulika katika kusaidia na kuwezesha watu wenye ulemavu wa macho nchini (CBM), Nesia Mahenge, ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya wiki ya AZAKi 2024, alisema kuwa kuelekea wiki hiyo maandalizi yamekamilika na kuwashukuru wadau wote waliojitokeza kudhamini na kuwezesha maadhimisho hayo.

Maadhimisho ya wiki ya AZAKi ni ya sita kufanyika tangu kuanzishwa kwake mwaka 2018.