SERIKALI imeagiza kuwa ulipaji fidia ya Sh. bilioni 6.2 kati ya Sh. bilioni 14.48 kwa wananchi 595 wa vijiji vinne katika Kata ya Engaruka mkoani Arusha, ufanyike kabla ya Februari 15, mwaka huu.
Wananchi wanaotarajiwa kunufaika na fidia hiyo ni wa vijiji vya Engaruka Chini, Mbaash, Idonyonado na Irerendeni wilayani Monduli na wanalipwa kwa ajili ya kupisha mradi wa magadi soda.
Akizungumza na wananchi wa eneo hilo, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Seleman Jafo, alisema fedha hizo za fidia zimetolewa ikiwa ni mkakati wa kutekeleza miradi huo wa kielelezo wenye manufaa makubwa katika kuendeleza sekta ya viwanda, kuongeza ajira, kukuza pato la taifa na uchumi kwa ujumla .
Pia aliliagiza Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC) kuhakikisha ulipaji huo unatendeka kwa haki na kufuatilia malalamiko yote ya wananchi yakayojitokeza na kushughulikiwa ipasavyo, kuandaliwa kwa mipango miji itakayoruhusu ujenzi wa hoteli na huduma nyingine za jamii.
Waziri Jafo pia aliwataka wananchi kuchangamkia fursa zitakazojitokeza kupata ajira na kuendeleza biashara.
Vilevile, alilisisitiza shirika hilo kusimamia upatikanaji wa wawekezaji wenye sifa na uwezo na si wababaishaji ili mradi huo ulete manufaa kwa taifa na wananchi kwa kurahisisha upatikanaji wa malighafi hiyo nchini na kuokoa fedha nyingi za kigeni zilizokuwa zinatumika kuagiza malighafi hiyo nje ya nchi.
Aidha, aliwasisitiza wananchi kupuuza taarifa potofu ambazo zimekuwa zikienezwa na watu ambao hawaitakii mema Tanzania wakivumisha kuwa mradi utaleta athari.
Jafo alisema NDC ambao ndio watekelezaji wa mradi huo wamekabidhiwa Cheti cha Tathmini ya Athari kwa Mazingira (EIA), kutoka Baraza la Taifa la Mazingira (NEMC) kinachothibitisha kuwa uchimbaji wa magadi soda katika eneo la Engaruka hauna athari zozote za kimazingira kwa ndege aina ya flamingo ambao wapo eneo hilo.
Dk, Jafo pia alisema serikali imeweka mpango wa kukahakisha eneo la Engaruka barabara zake zinapitika pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa umeme mkubwa KV 33 kwa ajili ya kuendesha viwanda sanjari na upatikanaji wa huduma za kijamii katika sekta za elimu, afya na maji safi na salama.
Aidha, viongozi mbalimbali walioshiriki hafla hiyo walisema mradi huo uliosubiriwa kwa takribani miaka 20, utakuwa kichocheo kikubwa cha maendeleo katika eneo hilo la Engaruka, Arusha na taifa kwa ujumla.
Naye Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geofrey Pinda, alisisitiza kuwa wizara yake itashirikiana na wananchi wa wilaya za Longido na Monduli kuweka mipaka na kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi katika vijiji vya Engaruka ili kuepuka migogoro.
"Wananchi wasigombanishwe na migogoro ya mipaka kati ya Wilaya za Longido na Monduli wekeni mipaka ili maendeleo yapatikane na wizara hii itatoa ushirikiano saa zote na RC Paul Makonda pale unapoona panakero tuwasiliane ili kutatua migogoro ili wananchi waishi kwa amani," alisema.
Aliwaelekeza maofisa ardhi katika wilaya za Monduli na Longido kushiriki kikamilifu katika zoezi la kurejesha mawe ya mpaka yaliyong'olewa na kupoteza utambuzi wa mpaka huo.
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo, Mariam Ditopile, aliipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kufanikisha jambo hilo ambalo limekaa muda mrefu na kuagiza fidia hiyo ilipwe kwa kuzingatia usawa na haki.
Naye Makonda alisema Arusha ni moja ya mikoa yenye bahati na kadri siku zinavyosonga, mkoa huo utatoa fursa mbalimbali za maendeleo kwenye sekta za kilimo, madini na michezo.
Alisema fursa hizo zitakazosaidia wananchi kujikwamua na umaskini na alihimiza wazawa wapewe kipaumbele wakati wa utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa kwenye Mkoa wa Arusha.
Akisoma taarifa ya utekelezaji wa mradi huo wa kimkakati, Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC, Dk. Nicolaus Shombe, alisema mradi huo umechukua zaidi ya miaka 20 tangu mchakato wake ulipoanza baada ya NDC kufanya utafiti.
Alisema NDC ilibaini uwapo wa magadi soda yenye mita za ujazo bilioni 3.8 sawa na tani milioni 787 ambapo kupitia utekelezaji wake, viwanda viwili vikubwa vitakavyogharimu Sh. trilioni 1.6 vitajengwa katika eneo hilo lenye ekari 60,884.
Dk. Shombe alisema viwanda mbalimbali vinatumia magadi soda hayo na Tanzania ni waagizaji wakubwa wa bidhaa hiyo kutoka nchi za Boswana na maeneo mengine huku ikitumia fedha nyingi za kigeni kuagiza.
Alisema mradi huo unaenda kusaidia kuokoa fedha za kigeni kwani badala ya kununua nje magadi hayo yatatokea eneo la Engaruka.
Vilevile, alisema elimu ya fedha imetolewa kwa wananchi waliopo eneo hilo na kwamba wananchi watakaolipwa fidia watatakiwa kuondoka katika eneo hilo ndani ya siku 90 zijazo.
Naye Mbunge wa Monduli, Fredrick Lowassa, alisema wananchi wana nyuso za furaha kutokana na fidia hiyo na kuiomba serikali kushughulikia changamoto za miundombinu zilizopo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED