Wahimizwa kupanga bei kwa vipimo sahihi

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 12:33 PM Jan 25 2025
Viazi.
Picha:Mtandao
Viazi.

WAKULIMA nchini wametakiwa kuwa huru kupanga bei ya kuuza mazao yao ya nafaka kwa kuzingatia thamani na vipimo sahihi ili kukuza uchumi wao kwa kupata mapato ya kutosha.

 Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Irene Mlola, katika mkutano wa wadau wa mazao ya nafaka ya dengu na choroko.

Mkutano huo umelenga kuwasaidia wakulima nchini kupata bei nzuri ya mazao hayo kipindi cha msimu wa mavuno.

Irene alisema COPRA imejizatiti kuhakikisha biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko yakiwamo hayo inafanyika kwa uwazi na haki.

Pia alisema vibali vya usafirishaji vitatolewa kwa wanunuzi waliosajiliwa na walionunua mazao hayo kupitia mifumo iliyoelekezwa na serikali.

“COPRA imejizatiti kuhakikisha biashara ya nafaka na mazao mchanganyiko inafanyika kwa kuzingatia haki, hivyo vibali vya usafirishaji vitatolewa kwa wanunuzi waliosajiliwa," alisisitiza.

Alisema lengo la COPRA ni kuona kila upande kati ya mkulima na mnunuzi wananufaika kiuchumi.

Irene aliwataka wakulima na wanunuzi kutumia fursa za uwapo wa mamlaka hiyo kuhakikisha wananufaika na kilimo cha mazao hayo yanayolimwa katika ukanda huo na maeneo mengine nchini.

Alisema serikali imewekeza katika sekta ya kilimo, hivyo wakulima wanapaswa kutumia fursa hiyo kuongeza uzalishaji wa mazao hayo na kupata faida kubwa zaidi.

Mkuu wa Mkoa huo, Evans Mtambi, aliwataka wananchi kuchangamkia fursa nyingi za kiuchumi zinazotokana na mnyororo wa thamani wa mazao hayo ya dengu na choroko kupitia mifumo iliyowekwa na serikali.

Mtambi alisema uwapo wa mifumo hiyo ya stakabadhi ghalani na minada ya mazao hayo ya kidigitali itawasaidia wakulima kuuza mazao yao kwa faida.

 “Kuwapo kwa mifumo ya stakabadhi ghalani kutawasaidia wakulima wa mazao hayo kuepuka kudhulumiwa katika vipimo, lakini kutachangia kupata faida,” alisema Mtambi.

Alisema mifumo hiyo itawasaidia wakulima kupata bei nzuri ya mazao yao na kuachana na ulaghai kutumia vipimo batili.