WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amesema serikali imeanza kupunguza deni la makandarasi la zaidi ya Sh. bilioni 300 kwa kulipa zaidi ya Sh. bilioni 145, huku kipaumbele kikiwa kwa wazawa.
Ulega alisema hayo jana jijini hapa wakati akikagua ujenzi wa vivuko vipya vitano kati ya sita vinavyoundwa na mkandarasi mzawa wa Kampuni ya Songoro Marine.
“Jambo la kipaumbele kwa Rais Samia Suluhu Hassan alilonipa mimi pamoja na Waziri wa Fedha, Dk. Mwigulu Nchemba, ni kuhakikisha hatulali usingizi mpaka tulipe madeni ya makandarasi hasa wa ndani.
“Wakati mimi ninakabidhiwa wizara hii Desemba, deni lilikuwa Sh. bilioni 300. Ndani ya mwezi mmoja, Rais Samia ameshusha deni hilo mpaka Sh. bilioni 200 na habari njema jana (juzi) amelipa Sh. bilioni 45 na sehemu ya fedha hizo zipo za makandarasi wa ndani,”alisema Ulega.
Alisema wanaamini ndani ya miezi miwili, deni hilo la ambalo limekuwa sugu kwa muda mrefu na likisemwa na makandarasi wa ndani, litakuwa limemalizwa.
“Matokeo yake ni kwamba barabara zilikuwa zimesinzia zitaanza kwenda mbio katika ujenzi wake, vilevile na uchumi wa Watanzania utazidi kuinuka kutokana na fedha hizo zinazolipwa kuongeza mzunguko wa fedha ndani,” alisema Ulega.
Kuhusu vivuko, Ulega alisema serikali inaendelea kutekeleza ujenzi wa vivuko vipya sita pamoja na ukarabati wa vivuko vitatu ndani ya Ziwa Victoria, Bahari ya Hindi, Ziwa Tanganyika na Nyasa kwa zaidi ya Sh. bilioni 56.
Pia alisema kati ya vivuko hivyo, vivuko vipya vitano vinavyotekelezwa katika Ziwa Victoria vinagharimu zaidi ya Sh. bilioni 50 na kati ya hivyo, vinne vinatarajiwa kukamilika kabla ya Machi, mwaka huu.
Alisema kivuko kimoja kinajengwa Dar es Salaam huku vinavyofanyiwa marekebisho ni pamoja na MV. Magogoni, MV. Kigamboni na MV. Nyerere.
“Nimpongeze mkandarasi huyu mzawa kwa kuendelea kufanya kazi nzuri na kuaminiwa na serikali kutekeleza miradi mikubwa na kufanikisha kwa uaminifu mkubwa,” alisema Ulega.
Awali, Mkurugenzi Mtendaji wa Songoro Marine Transport Ltd, Meja Bakari Songoro, alisema utekelezaji wa vivuko hivyo utakamilika hivi karibuni.
“Kivuko cha Bwiro-Bukondo chenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 kimefikia asilimia 91.3 kitakamilika Machi, 31 mwaka huu. Nyegezi-Busorya asilimia 84.5 kinakamilika Marchi 29, Nyakariro-Kome 83.19 kinakamilika Machi, 29, Buyagu-Mbarika 88 kinakamilika Julai 4,” alisema Songoro.
Alisema hadi vivuko vitano vya Ziwa Victoria kukamilika watakuwa wanaidai serikali Sh. bilioni 12.417.
Mbunge wa Sengerema, Khamis Tabasamu, alisema uhitaji wa vivuko katika eneo lake bado ni mkubwa.
Alisema kutekelezwa kwa kivuko cha Buyagu-Mbarika chenye uwezo wa kubeba abiria 200 na tani 100 za mizigo kitasaidia kupunguza vifo vya wananchi zaidi ya 30 wanaofariki dunia kila mwaka kutokana na tatizo la usafiri majini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED