Mv. Mwanza yaanza majaribio ya kwanza Ziwa Victoria

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 03:12 PM Mar 28 2024
MV. Mwanza "Hapa Kazi Tu" akiwa kwenye maji kwa ajili ya majaribio.

MELI ya Mv. Mwanza ‘Hapa kazi tu’ imefanya safari ya kwanza ya majaribio ya kiufundi katika Ziwa Victoria.

Majaribio hayo yatafanyika kwa siku tatu ili kubaini utendaji kazi wa mitambo iliyosimikwa ndani ya meli hiyo, jaribio hilo lilihusisha wataalamu 60 kutoka ndani na nje ya nchi.

Akizungumza baada ya meli hiyo kung’oa nanga katika Bandari ya Mwanza Kusini, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Eric Hamissi alisema safari hizo ni za majaribio ya kitaalamu kuelekea kukabidhiwa rasmi.

“Tunatarajia kufanya majaribio haya kwa muda wa siku tatu kulingana na atakavyoshauri mkandarasi mshauri baada ya kubaini mitambo hiyo inavyofanya kazi katika ubora uliokusudiwa kabla ya kumalizia sehemu iliyobaki ili Mei 31 tukabidhiwe rasmi kama ambavyo tumekubaliana kwenye mkataba,” alisema.

Hamissi alisema kukamilika kwa majaribio hayo kutapandisha asilimia za utekelezaji wa mradi huo hadi asilimia 96, huku akisisitiza kuwa zoezi hilo pekee linabeba asilimia tatu, huku asilimia nne zilizobaki zinamalizika Aprili na Mei.

Meneja Mradi, Vitus Mapunda alisema majaribio hayo yanahusisha uangalizi wa mitambo iliyofungwa ndani ya meli ili kuona ufanisi wake na ufanyaji kazi, ili kujihakikishia usalama wa meli.

Mapunda alisema meli hiyo imejengwa kumudu daraja la tatu la mawimbi katika bahari, limejengwa kumudu viwango vya bahari kuu na hata majaribio yake yanafanywa kwa kuzingatia ISO 19.

Ujenzi wa meli hiyo ulianza Januari 11,  2019 ukitarajia kukamilika Januari 10,  2021 lakini ulisogezwa mbele, kwamba hivi sasa unatarajiwa kukamilika na kukabidhiwa rasmi Mei 31 mwaka huu.