Muitikio ni mdogo watu wenye ulemavu kutembelea banda la REGROW Sabasaba- Mbura

By Grace Mwakalinga , Nipashe
Published at 02:02 PM Jul 10 2024
Ofisa Utalii  wa Mradi wa kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa  Tanzania (REGROW), Hoza Mbura, akitoa elimu  kwa wananchi waliotembelea bando hilo lililopo kwenye viwanja vya maonesho sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
PICHA NA GRACE MWAKALINGA
Ofisa Utalii wa Mradi wa kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW), Hoza Mbura, akitoa elimu kwa wananchi waliotembelea bando hilo lililopo kwenye viwanja vya maonesho sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.

OFISA Utalii wa Mradi wa Kuboresha Usimamizi wa Maliasili na Kukuza Utalii Kusini mwa Tanzania (REGROW), Hoza Mbura amesema tangu kuzinduliwa kwa maonesho ya 48 ya biashara kimataifa yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba jijini Dar es Salaam hadi sasa hakuna mtu mwenye ulemavu aliyefika katika Banda lao kwa ajili ya kujifunza au kupata taarifa zinazohusu masuala ya utalii.

Hoza ametoa kauli hiyo akizungumza na Nipashe digital kuhusu muitikio wa watu wenye ulemavu kutembelea Banda lao, kujifunza utalii unaopatikana kwenye mikoa ya kusini zikiwemo Hifadhi za Taifa kama vile Ruaha, Nyerere na Kitulo, utalii wa utamaduni na kilimo.

Amesema watu   500 wakiwemo watoto,wanawake na wanaume, wametembelea banda la REGROW,kujionea shughuli mbalimbali zinazofanywa na mradi huo katika kuboresha miundombinu na kukuza utalii.

“ Ni  muhimu kwa makundi ya watu wenye ulemavu kutembelea maonesho ya kibiashara Sabasaba  kupata taarifa ambazo zitawasaidia kufahamu shughuli zinazofanywa kwenye sekta ya utalii ili kujua  maeneo gani ya kutembelea,” amesema Hoza.

Ameongeza kuwa lengo la REGROW ni kuongeza  ubora wa vivutio vya utalii  kwenye maeneo yenye kipaumbele ukanda wa  Kusini mwa Tanzania na kuimarisha usimamizi wa maliasili, kuongeza fursa za  kiuchumi kwa wananchi wanaozunguka hifadhi za kipaumbele na kuboresha na  kuimarisha usimamizi wa vyanzo vya maji.

Hoza Mbura Ofisa Utalii kutoka REGROW akitoa elimu kwa watoto waliotembelea banda hilo kwenye maonesho ya kibiashara viwanja vya sabasaba jijini Dar es Salaam, namna mradi huo unavyosaidia kukuza sekta ya utalii Nchini.PICHA NA GRACE MWAKALINGA

Akizungumza baada ya kutembelea mabanda yaliyopo Wizara ya Maliasili na Utalii, aliyekuwa Katibu Mkuu Mstaafu wa Wizara hiyo, Balozi Mstaafu Meja Jenerali, Gaudence Milanzi amefurahishwa namna wizara hiyo imeweka vitu mbalimbali vya utalii na elimu ya masuala ya utalii na uhifadhi.

Amesema wizara hiyo inafanya kazi  nzuri inayoshawishi watalii kutoka ndani na nje ya nchi kujionea vivutio vya utalii vilivyopo Tanzania, amewaomba wadau kuunga mkono jitihada hizo ili kukuza sekta ya hiyo.

Jesca Ambele, mkazi wa Gongo la Mboto ambaye ametembelea banda la REGROW amesema maonesho ya biashara yanatoa fursa kwa wananchi kujifunza masuala mbalimbali.