WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema serikali imefufua viwanda vingi katika Mkoa wa Tanga vikiwemo vya kuchakata zao la mkonge ikiwa ni jitihada za kuvirejesha na kuwezeshwa kuingia kwenye uchumi wa viwanda.
Majaliwa alitoa kauli hiyo wakati akiweka jiwe la msingi kwenye mradi wa jengo la kitega uchumi la Halmashauri ya Jiji la Tanga ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Muungano wa Tanzania yatakayofanyika kesho.
"Tumefufua viwanda vingi vya mkonge, zao ambalo lilikufa kabisa katika wilaya zote mkoani hapa, sasa serikali ya awamu ya sita imekusudia kuvifufua ili kuingia kwenye uchumi wa viwanda, " alisema.
Aliwataka wakazi wa Tanga kuchangamkia fursa za uchumi wa buluu kutokana na mkoa huo kuwa na uwezo mkubwa wa kusafirisha shehena zinazotokana na bahari.
Majaliwa, alisema idadi ya wavuvi ni ndogo ikilinganishwa na eneo la bahari, hivyo hakuna sababu ya kuacha kutumia fursa hizo na kutumia bahari hiyo vizuri.
"Serikali yenu imeamua kujenga bandari kubwa ya uvuvi wilayani Kilwa (Mkoa wa Lindi) kwa sababu bahari ile pamoja na bahari kuu inatoa samaki maarufu Duniani anayeitwa 'Tuna' na ana bei kubwa, kwa hiyo kwa kuweka bandari ile tulikuwa tunashawishi pia wawekezaji wenye meli zinazovua bahari kuu waje wavue," alisema.
Alifafanua kuwa Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliondolewa kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi ili kuipa wepesi wa kuratibu shuhuli zake pasipo muingiliano.
"Na mimi sina shaka wote mnafahamu manufaa ya uvuvi sababu mko karibu na bahari, kiwango cha ulaji wa samaki nchini kimepungua, lakini siyo kweli samaki wamepungua baharini bali wajasiriamali wanaotaka kujikita kwenye uvuvi ndiyo wamepungua, samaki tunao lakinu tunashindwa kwenda kuvua," alisema Waziri Mkuu.
Kufuatia hali hiyo, alisema katika kipindi cha miaka mitatu, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan amenunua boti za kisasa za kuvulia 222 na kuanza kuzigawa mikoa ya Kanda ya Ziwa, ikifuatiwa na ya Pwani, Tanga, Dar es Salaam na Lindi ili wajasiriamali wote wapate na kuzitumia kujiingizia kipato.
Majaliwa aliwaagiza wakuu wa wilaya zote zilizopo mwambao wa bahari hiyo kuwahamasisha wananchi wavuvi kujikita katika uvuvi na kutumia fursa kupitia uchumi wa bluu.
Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Balozi Dk. Batilda Buriani, alisema mkoa huo wa kimkakati hususani kupitia zao la mkonge, hivyo serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo kuendeleza kilimovili ni kukuza uchumi.
"Kama tunavyojua mkoa wetu unaenda kupanuka kiuchumi kutokana na maboresho makubwa yaliyofanywa na Rais wetu, tuendelee kuimarisha uchumi kupitia zao la Mkonge na viungo ikiwa ni pamoja na kutumia fursa za uchumi wa buluu ili kufungua uchumi," alisema Batilida.
Akitoa salamu za chama, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa Mkoa huo, Rajab Abdallah, alisema wananchi mkoani humo wana amani ambayo inalindwa na serikali yao.
"Thamani ya amani katika nchi yetu ni kubwa sana na sisi Wanatanga tumejipanga vya kutosha kuhakikisha kwenye Uchaguzi Mkuu mwaka 2025 Tanga tutaongoza kwa kura za Rais nchi nzima,
"Hii ni kutokana na maendeleo makubwa yanayofanyika katika uwekezaji mkubwa wa fedha za serikali kwenye mambo mbalimbali ya kimandeleo, tunayo sababu ya kuendelea kumuunga mkono Mheshimiwa Rais wetu kwa kazi kubwa anayoifanya," alisema Abdallah.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED