WAKATI kikosi cha Simba kikitua salama nchini Tunisia tayari kwa mchezo wao wa marudiano wa Kombe la Shirikisho hatua ya makundi dhidi ya CS Sfaxien, Kocha wa timu hiyo, Fadlu Davids amesema wapo tayari kwa mchezo huo na wachezaji wake watapambana dakika zote.
Simba Jumapili itacheza mchezo huo muhimu ugenini kujaribu kusaka pointi tatu zitakazowaweka kwenye mazingira mazuri ya kufuzu hatua ya robo fainali ya michuano hiyo.
Akizungumza muda mfupi baada ya kutua nchini humo, Fadlu, alisema hawana cha kuhofia katika mchezo huo kikubwa wanapaswa kucheza kwa malengo waliyojiwekea kuweza kupata ushindi.
"Nafahamu hautakuwa mchezo mwepesi, lakini lazima tupambane kuhakikisha tunapata ushindi, wapinzani wetu najua wamejipanga kujaribu kulipa kisasi kwa kufungwa mchezo wa kwanza, lakini tumejiandaa kuwakabili," alisema Fadlu.
Aidha, alisema pamoja na kuhitaji ushindi, watacheza kwa tahadhari mchezo huo na kuwa na nidhamu ya ulinzi huku wakipanga mashambulizi yao vizuri.
Katika hatua nyingine, Meneja Habari wa klabu hiyo, Ahmed Ally, alisema kikosi cha timu hiyo kimetua salama nchini humo huku kila mchezaji akiwa na morali na mchezo huo.
"Wanasimba waliobakia nyumbani waiombee timu yao kuweza kupata ushindi, ni mchezo mzuri na kila mchezaji anafahamu umuhimu wake, tumekuja kuwashangaza waarabu nyumbani kwao," alisema Ahmed.
Alisema katika mazungumzo yake na wachezaji wa timu hiyo, kila mmoja ameonyesha kuwa na shauku na kuitamani mechi hiyo ya Jumapili.
"Wachezaji wana morali sana, kila mmoja mawazo yapo kwenye mchezo huu, wanafahamu umuhimu wa ushindi, mchezo huu ni muhimu sana kwetu kwenye harakati za kuingia robo fainali, matokeo tutakayoyapata hapa yatatupa taswira kamili ya safari yetu kuelekea robo fainali," alisema Ahmed.
Kwenye kundi lao Simba ina pointi sita sawa na Bravo do maquiz ya Angola, CS Costantine huku Cs Sfaxien wakiwa hawana pointi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED