NYOTA wa klabu ya Yanga, Max Nzengeli na Khalidy Aucho kwa nyakati tofauti wamesema kwa wachezaji wazawa hapa nchini, kiungo wa Azam FC na timu ya taifa 'Taifa Stars', Feisal Salum 'Feitoto' ni mmoja wa wachezaji wenye kipaji na uwezo mkubwa.
Akizungumza jijini Dar es Salaam, Nzengeli alisema kwa wachezaji wa ndani, Feitoto ni mchezaji anayejua mpira na ana uwezo mkubwa.
"Anaweza kucheza popote, ni mchezaji mzuri sana, nadhani watanzania wanatakiwa kujivunia kuwa naye ingawa wapo wachezaji wengine wengi wenye uwezo," alisema Nzengeli ambaye hivi karibuni mchezaji wa Simba, Ladack Chasambi alinukuliwa akimtaja kama mchezaji 'kioo' kwake hapa nchini.
Aidha, mbali na Feitoto, Nzengeli pia amemtaja kiungo wa Simba, Awesu Awesu kuwa ni miongoni mwa wachezaji wenye uwezo mkubwa.
Kwa upande wake, Aucho, mchezaji wa kimataifa wa Uganda, naye alisema pamoja na Tanzania kuwa na wachezaji wengi wenye vipaji na uwezo mkubwa, kwake Feitoto anakaa juu yao.
"Ana uwezo mkubwa sana miongoni wa wachezaji wa Tanzania, huwa namfuatilia akicheza kwenye timu yake ya Azam FC," alisema Aucho.
Kabla ya kujiunga na Azam FC msimu uliopita, Feitoto alikuwa akiichezea Yanga waliomsajili kutoka Singida United wakati ikishiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kabla ya kushuka daraja.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED