MBUNGE wa Mpanda Mjini, Sebastian Kapufi amewashauri viongozi wa kisiasa wakiwamo wabunge, wenyeviti wa halmashauri na madiwani wenye kampuni za ujenzi kutokuwa sehemu ya waombaji wa zabuni za miradi ya maendeleo ya halmashauri husika.
Amesema wakishiriki watakuwa wanaathiri utekelezaji wa miradi hiyo na thamani ya fedha iliyotolewa inashindwa kuonekana katika miradi husika inapokamilika.
Alitoa ushauri huo juzi alipokuwa katika ziara ya kikazi iliyolenga kukagua miradi ya maendeleo iliyofanyika katika kata zote za Jimbo la Mpanda mjini, mkoani Katavi.
Kapufi alisema wananchi wanatamani kuona kuna uwiano sawa wa fedha zilizotolewa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika halmashauri hiyo ambayo serikali imepeleka zaidi ya Shilingi bilioni sita katika msimu wa fedha wa mwaka 2024/25.
"Mathalani imetolewa Sh. milioni 600 kwenye ujenzi wa mradi wa shule ya sekondari ni vyema hata mwananchi wa kawaida akaona thamani ya mradi huo ikifanana na fedha zilizotumika sio kuwapo na ujanja ujanja ambao unafanya miradi mingi kutekelezwa chini ya kiwango," alisema.
Kadhalika, viongozi hawapaswi kuwa sehemu ya washiriki katika shughuli hizo, kwa kuwa kufanya hivyo kutafanya washindwe kutimiza wajibu wao wa kusimamia utekelezaji wa miradi hiyo.
Kauli ya Kapufi inakuja wakati baadhi ya viongozi wa kisiasa ni miongoni mwa wamiliki wa kampuni za ujenzi na wamekuwa wakitajwa kushinda zabuni za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo, ambayo mingine ikilalamikiwa kutekelezwa chini ya kiwango.
Awali, Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda, Leonard Kilamhama, alisema serikali imetoa Sh. bilioni 4.7 kwa ajili ya ujenzi wa shule mbili za Shanwe na ya kanda itakayochukua wanafunzi kutoka mikoa ya Katavi, Kigoma na Tabora.
Kilahama alisema kukamilika kwa ujenzi wa shule hizo kutasaidia kupunguza tatizo la wanafunzi kukosa nafasi za masomo wanapofaulu mitihani yao ya mwisho ya kumaliza elimu ya msingi.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED