RAIS mstaafu Jakaya Kikwete amekiri kuvutiwa na mchango mkubwa wa Benki ya NMB wa Sh. bilioni moja kati ya Sh. bilioni 2.71 zilizokusanywa wakati wa hafla ya kuchangisha fedha za matibabu ya watoto 1,500 wanaotibiwa na Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Kikwete alitoa pongezi hizo mwishoni mwa wiki wakati wa hafla hiyo iliyoandaliwa na JKCI kwa kushirikiana na Heart Team Africa Foundation (HTAF), lengo likiwa kukusanya fedha za matibabu ya watoto wasio na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Kikwete alisema Sh. bilioni moja zilizotolewa na NMB, iliyotia saini makubaliano ya ushirikiano na JKCI ya kutoa kiasi hicho kwa miaka minne, kinakwenda kuongezea nguvu serikali inayopambania uamuzi wake wa kisera wa kuendelea kujenga uwezo wa ndani wa kutibu maradhi ya moyo.
"Gharama za kupeleka wagonjwa nje ni kubwa sana na huu ulikuwa ndio msukumo uliozaa uanzishwaji wa JKCI, leo taasisi imefikia hatua kubwa na bora katika matibabu ya moyo, ambayo serikali inagharamia asilimia 70 ya matibabu na familia kuachiwa asilimia 30 (sawa na Sh. milioni nne kwa mtoto), ambayo pia ni kubwa kwa walio wengi.
"Nimevutiwa na michango ya wadau wa afya, kipekee sana kwa mchango wa NMB. Pesa alizochangia dada’angu Ruth Zaipuna (Ofisa Mtendaji Mkuu wa NMB), ni nyingi mno, Sh. bilioni moja walizotoa zinakwenda kuokoa maisha ya takribani watoto 250 kati ya 1,500, wakiwamo 500 wanaohitaji operesheni ya haraka," alisema Kikwete.
Kikwete alipongeza serikali za awamu ya tano na sita kwa kuendelea kuwekeza katika shughuli za JKCI na kugharamia asilimia 70 za gharama za matibabu, ambapo taasisi imeendelea kuimarishwa kwa vifaa vya kisasa, huku akiwataka wadau zaidi kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali.
Akizungumza kabla ya kukabidhi hundi ya mfano yenye thamani ya Sh. bilioni moja, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NMB, Zaipuna, alimpongeza Rais mstaafu Kikwete kwa maono yake yaliyolenga kutatua changamoto za watanzania wanaosumbuliwa na magonjwa ya moyo na kuanzisha JKCI, ambayo sasa imekuwa tegemeo ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
"Benki ya NMB ipo hapa kuungana na wadau wetu katika maendeleo ya kijamii ili kuunganisha nguvu zitakazoleta nuru kwa watoto wetu, kwa kugusa mioyo yao na kuwatia matumaini kwa kuendelea kufanikisha upatikanaji huduma bora na nafuu za kitabibu, hasa kwa watoto wenye changamoto za moyo.
"Katika kuunga mkono jitihada hizi, hivi karibuni NMB tumetia saini makubaliano ya kuchangia Sh. bilioni moja katika kipindi cha miaka minne na leo tuko hapa kukabidhi hundi ya mfano yenye thamani hiyo, tukiamini kwamba mchango wetu utakuwa msaada mkubwa hasa kwa wazazi wanaoshindwa kumudu gharama za matibabu ya watoto wao.
"Licha ya mchango huu, NMB itashirikiana na JKCI, kuwezesha wataalamu wa taasisi hii kutoa elimu ili kuongeza ufahamu wa afya ya moyo kwa watanzania, pia tutawajibika kushiriki shughuli mbalimbali za upatikanaji fedha za matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo JKCI," aliahidi Zaipuna.
Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk. Peter Kisenge mbali na kumpongeza Rais mstaafu kwa maono yaliyozaa taasisi hiyo na uwekezaji mkubwa aliofanya wakati wa uongozi wake, alisifu mapinduzi makubwa ya kihuduma na kimfumo yaliyofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan anayeungwa mkono na wadau, ikiwamo NMB.
"Tunamshukuru Rais Samia kwa kuhakikisha 4R zake zinafanya kazi nzuri katika nyanja zote, lakini pongezi za kipekee ni kwako Rais mstaafu kwa kuwezesha wazo la kuwa na taasisi hii ambalo lilikuwapo tangu enzi za Rais wa Kwanza Julius Nyerere, lakini likakwama. Wewe ukaliibua na kulifanikisha.
"Ukajenga taasisi hii kwa msaada wa Serikali ya China, serikali yako ikitoa Sh. bilioni 11 na Serikali ya China ikitoa Yuan bilioni 18 na kufanikisha ujenzi wa JKCI ambayo imekuwa suluhu ya changamoto za moyo Afrika Mashariki, ambako tayari tumeshafanya zaidi ya operesheni 688,00 tangu mwaka 2015 ilipoanza," alisema.
Mwenyekiti wa Bodi ya HTAF ambaye pia ni Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Mussa Zungu, alimshukuru Rais mstaafu Kikwete na kusema mchango wa kiongozi huyo wa zamani kwa sekta ya afya, hasa watoto wenye magonjwa ya moyo ni wa kipekee.
"Maono yako yameacha urithi wa kweli kupitia wazo lako la uanzishwaji JKCI, ambayo imekuwa kimbilio la wengi si tu hapa nchini, bali pia Afrika Mashariki na Kati. Hakika wewe ni mfano wa kiongozi anayejali afya za watu wake na kinachofanyika hapa ni mwendelezo utokanao na maono yako.
"Shukrani za dhati kwa Rais Samia katika kuboresha si tu miundombinu na vifaa tiba, bali pia kukubali kuchangia asilimia 70 ya gharama za matibabu ya watoto, ambao wanachangiwa katika hafla hii kupata asilimia 30 ya gharama hizo. Tunashukuru NMB kwa mchango wa Sh. bil. moja, lakini pia kwa washiriki na wachangiaji wote," alisema Zungu.
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED