Halmashauri zabanwa upandaji miti, ATCL yatia mguu

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 07:29 PM Mar 28 2024
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo akiwa pamoja na wanafunzi wakupanda miti.
PICHA: VITUS AUDAX
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo akiwa pamoja na wanafunzi wakupanda miti.

Halmashauri nchini zatakiwa kuhakikisha zinatekeleza lengo la upandaji miti milioni 1.5 kama yalivyo maelekezo ya serikali kwa kushirikiana na Wakala wa Misitu Tanzania (TFS).

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Selemani Jafo, wakati wa uzinduzi wa mradi wa utunzaji mazingira wa Twiga wa kijana unaogharimu zaidi ya Sh.milioni 124.

Kwa mujibu waziri huyo, mradi wa Twiga na Kijana utakuwa sehemu ya utekelezaji wa kampeni ya upandaji mti iliyoanzishwa mwaka 2022, ikijulikana n a ‘Soma na Mti,’ ikiwa na lengo la kutoa elimu kwa vijana na wanafunzi, juu ya umuhimu wa upandaji miti.

Jafo amesema kuwa katika hatua hiyo ya kupandikiza elimu hiyo ya upandaji miti kwa wanafunzi ambayo inaambatana na shughuli za upandaji miti, ina lengo la kupunguza uchafuzi mazingira utokanao na hewa ya kaboni pamoja na mabadiliko ya tabia nchi.

Hivyo amezitaka halmashauri hizo 184, kutenga bajeti kwa ajili ya kuwawezesha wanawake pamoja na vikundi mbalimbali vya uzalishaji miti, ili kuongeza idadi ya miti nchini na kukabiliana na ongezeko la joto ulimwenguni.

Pia imeelezwa kuwa safari za anga ni sehemu ya uzalishaji wa hewa ya kaboni kwa asilimia 2.4 hadi 2.5, na kwamba uchangiaji huo wa kaboni unatarajiwa kuongezeka zaidi ifikapo 2023 hadi kufikia asilimia tano, huku ukichangia pia ongezeko la joto ulimwenguni.

Kwa muktadha huo, ndipo shirika la ndege Tanzania (ATCL), limeamua kuufadhiri mradi huo wa Twiga na Kijana.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo ambayo inayosimamiwa na shirika lisilokuwa la kiserikali la Wezesha Binti na Mama Mjasiriamali (WBM), Radislaus Matindi, mkurugenzi mtendaji wa ATCL, amesema kuwa ufadhili huo ni sehemu ya juhudi za shirika hilo kupunguza ongezeko la joto na hewa ya kaboni nchini.

Aidha, Matindi amesema shirika hilo linaendelea na mapambano ya mabadiliko ya tabia nchi kwa kujikita zaidi katika matumizi ya mifumo rafiki ya injini pamoja na kufadhiri miradi ya utunzaji wa mazingira kwa fungu la zaidi ya Sh.milioni 124 utakaotekelezwa kwa kipindi cha mwaka mmoja.

Kwa upande wa Ratifa Mohamedi, mkurugenzi wa WBM, amesema kuwa kampeni hiyo inalenga kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira kwa wanafunzi wa shule 60 ambazo ni za msingi na sekondari; pamoja na kupanda miti 6,000 katika mikoa sita.

Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Mwanza, Kagera, Kilimanjaro, Mbeya, Arusha na Mtwara ambapo kila mkoa watapanda miti 1,000 kwa shule 30 za msingi na 30 za sekondari.

“Shule na mikoa husika imechaguliwa kutokana na umuhimu wake pamoja na kuwa mikoa hiyo ni sehemu ambako ATCL inatekeleza safari zake,” amesema na kuongeza;

“Pia tutatoa elimu kuhusu shughuli zinazotekelezwa na shirika hili ikiwa ni pamoja na ofa zinazotolewa kwa watu mbalimbali wakiwemo wanafunzi.”