DC Ileje awataka wanufaika TASAF kujinusuru na umaskini

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 05:42 PM Nov 15 2024
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi.
Picha:Mpigapicha Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi.

Mkuu wa Wilaya ya Ileje, Farida Mgomi, amewahimiza wanufaika wa Mpango wa Kunusuru Kaya Masikini (TASAF) katika Kata ya Mlale kuzitumia vizuri fedha wanaozipata.

Amewataka kutumia fedha hizo kwa kuwekeza katika shughuli za maendeleo ili kuweza kujinusuru katika wimbi la umasikini.

Akizungumza katika Kijiji cha Yuli kilichopo katika Kata ya Mlale wilayani humo, Mgomi amewasistiza wanufaika wa mradi huo kuzitumia fedha za TASAF kwa matumizi yaliyokusudiwa na serikali ili pale watakapohitimu katika mpango huo,wawe wamenufaika.

Amewataka pia kuwa sehemu ya kutimiza azma ya mpango huo wa serikali kwa kujiondoa katika wimbi la umasikini.

Vilevile Mgomi, amemwagiza Katibu Kata, Watendaji wa Vijiji, Maafisa Ugani na Idara ya Maendeleo ya Jamii kuweka mpango maalum wa wanufaika kuvitunza, kuimarisha na kuviendeleza vikundi vyao.
Amesema lengo ni  kujikimu kimaisha na kuendeleza shughuli za maendeleo ikiwa ni pamoja na kunufaika na mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo.

Mgomi pia amemshukuru Rais  Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujali na kuziinua kaya masikini kupitia Mpango wa TASAF ambao mpaka sasa kaya mbalimbali katika Wilaya ya Ileje zimenufaika.