ATCL yaingia mkataba mashirika makubwa ndege kusafirisha watalii

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 06:34 AM Apr 18 2024
Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).
Picha: Maktaba
Ndege ya Shirika la Ndege Tanzania (ATCL).

BUNGE limeelezwa kuwa Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), limeingia mikataba ya ushirikiano wa kibiashara na mashirika makubwa ya ndege ya kimataifa kwa ajili ya kusafirisha watalii kwenye maeneo ambayo mashirika hayo hayafiki.

Mashirika hayo ni pamoja na Qatar, Emirates, KLM, Air India, Ethiopia na Oman Air, ambayo huleta watalii Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA) na Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Kilimanjaro (KIA).

Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, alisema hayo bungeni jana alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Shaurimoyo (CCM), Ali Juma Mohamed.

Mbunge huyo alitaka kujua sababu gani zinafanya ATCL isitumie fursa ya kubeba watalii wanaotoka nchi mbalimbali duniani kuja nchini.

Akijibu swali hilo, alisema ATCL inatumia fursa iliyopo ya kusafirisha abiria wakiwamo watalii kwa kuanzisha vituo vilivyo karibu na vituo vya utalii nchini kama vile kituo cha Kilimanjaro na Arusha kwa watalii wanaotembelea Hifadhi ya Ngorongoro, Hifadhi ya Ziwa Manyara, Hifadhi ya Tarangire na Mlima Kilimanjaro.

Kituo cha Mwanza kuna hifadhi ya Serengeti, kituo cha Zanzibar kuna fukwe za bahari, hifadhi ya ghuba ya Johazi, msitu wa Pogwe pamoja na maeneo ya kihistoria.

Kituo cha Kigoma kuna hifadhi ya Gombe, kituo cha Mpanda kuna hifadhi ya Katavi na kituo cha Iringa kuna hifadhi za Mikumi, Ruaha na Kitulo.