ZAIDI ya abiria 300,000 wamesafiri kwa treni ya Reli ya Kisasa (SGR) ndani ya siku 44, hivyo kufanya hadi sasa idadi ya waliopanda tangu ianze huduma kati ya Dar es Salaam na Dodoma Agosti, 2024 kufikia watu milioni 1.5.
Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, aliyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari katika stesheni ya Dodoma ambao walikuwa wakijiandaa kusafiri kwenda katika mkutano wa msemaji huyo utakaofanyika leo Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Morogoro.
Msigwa alisema takwimu hizo zinaonesha ni wastani wa abiria 300,000 kwa mwezi wanasafiri na kusisitiza kuwa, zipo treni za kutosha kutoa huduma ya usafiri kwa wananchi.
Alisema vichwa vya treni 17 na mabehewa zaidi ya 78 yameingia na serikali imejipanga kutoa huduma ya vizuri kwa wananchi.
“Matatizo yanayojitokeza kwenye usafiri huu ni ya kawaida lakini pia, kuna hujuma za miundombinu tumeendelea kuchukua hatua na kuhusu umeme tatizo linalojitokeza mara moja, linatokana na shida Gridi kwenye yote ya Taifa,” alisema.
Alisema serikali inaendelea na ujenzi wa vipande vingine kwa awamu na lengo ni kukamilisha mradi huo ili kutoa huduma na utakapokamilika utakuwa umegharimu Sh. trilioni 23.
Hata hivyo, alisema serikali inakamilisha maandalizi ya kuanza kusafirisha mizigo kwa kipande mikoa ya Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam.
Msigwa alisema treni moja itakuwa na uwezo wa kubeba tani 10,000 na tayari mabehewa 264 yamewasili na mengine 264 yapo bandarini wakati wote yatashushwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED