Watimuliwa, wafungiwa kuingia nchini kwa madai kuhamasisha ushoga

By Augusta Njoji , Nipashe Jumapili
Published at 10:46 AM May 19 2024
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni.
Picha: Maktaba
WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni.

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, amesema hadi sasa watu 64 wa mataifa mbalimbali na jumuiya zilizokuwa na viashiria vya mmomonyoko wa maadili, ikiwamo ushoga wametimuliwa na kufungiwa kuingia nchini.

Aidha, wakimbizi 41 wamewekewa zuio la kuingia nchini kutokana na kuhamasisha vitendo hivyo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Hamad Yusuf Masauni, amesema hayo bungeni wakati akichangia na kujibu hoja zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka 2024/25.

Katika mjadala huo, wabunge walitaka mkakati wa serikali kudhibiti vitendo vya  ushoga, ulawiti na ubakaji.

Akijibu hoja za wabunge, Masauni amesema serikali haipo kimya katika kupambana na vitendo hivyo na imeendelea na vita ya kisayansi kukabiliana navyo.

“Waheshimiwa Wabunge wameonyesha uchungu katika eneo la mapambano dhidi ya ushoga, na vita dhidi ya unyanyasaji wa kijinsia , nakiri kwamba vita hii ni pana sana, ni kubwa na mapambano dhidi ya vita hii ni lazima tushikamane kama nchi ili tuweze kushinda,”amesema.

Amefafanua kuwa Jeshi la Polisi linapambana kupitia sheria dhidi ya uhalifu huo ambao umeidhinishwa katika sheria zilizopo nchini ni kuwa kubaka, kulawiti, shambulio la aibu, kuzini, kumpa mimba mwanafunzi ni uvunjaji sheria namba 12 ya marekebisho ya mwaka 2022.

Amesema makosa ya ushoga, ipo kwenye sheria ya makosa ya maadili ya jamii hivyo kimsingi kupitia sheria hizo kuna mambo yamefanyika ikiwemo kuwachukulia watu wanaofanya hivyo hatua kwa kuwaondoa nchini ambao wanaleta habari ambazo hazipo katika misingi ya mila, sheria na utamaduni wa kitanzania.

Kuhusu adhabu na dhamana, amesema ni masuala ya kisheria na kwamba bunge ndio lina mamlaka ya kufanya mabadiliko hivyo serikali imepokea hoja hiyo ya msingi  watakaa pamoja kutafakari kama kuna haja ya kuangalia sheria hizo ili zifanyiwe maboresho.

Kwac upande wa Idara ya Uhamiaji, amesema ana orodha wa watu 64 ambao wametimuliwa nchini na kuwapiga marufuku kuingia nchini kutoka mataifa mbalimbali waliogundulika kwamba wana viashiria vya ushoga.

“Pia wako  wakimbizi 41 wamepigwa Prohibited Immigrant (kuzuiwa mipakani wasiingie nchini) ni marufuku kuingia katika nchi hii, kwahiyo kazi hii inaendelea, taasisi vilevile jumuiya zinazosajiliwa kuna ambazo zimefungiwa hivyo kuna hatua ambazo zinachukuliwa na kila sehemu katika kupambana na vita hii,” amesema .

Naye, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Jumanne Sagini, amesema serikali imekuja na mkakati wa kulinda ushahidi dhidi ya wanaofanyiwa vitendo vya ubakaji, ulawiti mahakamani ambapo kwa sasa kesi inaposajiliwa siku hiyohiyo maelezo ya awali ya mlalamikaji husokwa, ili huko mbele yasibadilishwe kwa familia kuamua kumalizana.

Sagini amesema katika kipindi cha kuanzia Januari, 2023 mpaka Mei, 2024, jumla ya mashauri 8,346 ya ukatili wa kijinsia yalisikilizwa katika Mahakama za Wilaya na Hakimu Mkazi.

“Kati ya mashauri hayo, mashauri 5,668  yalikwisha. Aidha, katika mashauri yaliyokwisha mahakamani, mashauri 2,420 yalikwisha kwa watuhumiwa kutiwa hatiani na mashauri 1,005 yalikwisha kwa watuhumiwa kuachiwa chini ya kifungu 225(5) kutokana na sababu mbalimbali,” amesema. 

Amezitaja sababu hizo ni waathiriwa wengi wa matukio ya ukatili wa kijinsia kuwa wanafamilia na hivyo baada ya kutoa taarifa na polisi wakiwa na jazba na baada ya hasira kuisha hukaa na kuimaliza kesi katika ngazi za familia na familia kusaidia.

Aidha, waathiriwa au wanafamilia hasa wazazi kupokea fidia na kukataa kutoa ushirikiano pindi kesi inapoanza kusikilizwa mahakamani

Pia, waathiriwa wenye umri kati ya miaka 15 mpaka 17 kutokuwa tayari kutoa ushahidi pindi wanapofika mahakamani au kukataa kabisa kufika mahakamani

Vilevile, kuhama shahidi kutoka sehemu moja kwenda sehemu nyingine bila kuacha mawasiliano kwenye vyombo husika.

“Hizo ni baadhi ya sababu ambazo, zinaweza zikapelekea wabunge kuhisi kwamba hatua hazichukuliwi, lakini tumeona ni mwenendo wa kijamii, mahakama zetu zimebaini tatizo ambapo mwanzoni mtu anaenda anaongea halafu hatua anageuka mbele.”

Amesema ili kukabiliana na hali hiyo mahakama imekuja na mkakati ambao ukitekelezwa upasavyo utasaidia kuwatia hatiani wote wanaothibitika kufanya makosa hayo.

“Imebainika baada ya shauri kuandikishwa, kesi inapotajwa wanafamilia wengi wanaporudi nyumbani wakija sio wale waliokuja na jazba siku ya kwanza wanatoa ushahidi usiweza kumfikisha mahakama, hivyo mahakama imekuja  na mkakati wa kesi inaposajiliwa siku ileile inasoma maelezo yote ya awali ya mlalamikaji ili huko mbele yasiweze kubadilishwa,”

Amesema hizo ni juhudi za vyombo vinavyotoa haki vinavyoonesha kukerwa na tabia hiyo ndio maana mahakama imeanza kuchukua hatua.

WAZIRI GWAJIMA

Akihitimisha hotuba yake, Waziri wa Wizara Dk. Dorothy Gwajima amesema michango iliyotolewa na wabunge kwake ni petroli ya kupeleka mbele mapambano dhidi ya vitendo hivyo vya ushoga na mapenzi ya jinsia moja.

“Moyo unaniuma nalia, silali na watanzania ni mashahidi nimechukulia kwa uzito na kusema sitaki ushoga ni marufuku through my dead body, nilikosa hii tone, lakini kwa tone hii…kazi kubwa itafanyika kwa sababu nyumba zinajulikana na watu wanajulikana, tutawadaka na hatua zitachukuliwa,”amesema.