Wachungaji wanaopinga ukeketaji wadai kutishiwa maisha Mara

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 11:05 AM Apr 21 2024
Wachungaji wanaopinga ukeketaji kutishiwa maisha.
PICHA: MAKTABA
Wachungaji wanaopinga ukeketaji kutishiwa maisha.

BAADHI ya wachungaji kutoka kata mbalimbali wilayani Tarime, mkoani Mara wameomba Jeshi la Polisi kuwachukulia hatua baadhi wa watu wanaotishia maisha yao kutokana na kupinga ukatili wa kijinsia ikiwamo ukeketaji.

Wachungaji na viongozi kutoka vyama vya siasa katika mji wa Sirari walifanya kikao cha pamoja na Jeshi hilo kujadili njia mbalimbali za kukabili uhalifu ikiwamo ukatili wa kijinsia.

Baadhi ya wajumbe wameonesha kushangazwa na kuongezeka vitendo hivyo licha ya kutungwa sheria kadhaa kwa ajili ya kukomeshwa ukatili huo unaokadiriwa kufanyiwa wasichana zaidi ya 2,000 wilayani humo.

Mchungaji Julius John ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza za Kipentekoste Tanzania (CPCT), wilayani Tarime ameomba mkuu wa polisi wilaya ya kipolisi Sirari yenye kuhudumia kata zote Jimbo la Tarime vijijini, afanye uchunguzi na kuchukua hatua.

"Hivi sasa baadhi ya wachungaji kutoka kata za Pemba na Mbogi wanatishiwa maisha yao kutokana na kukemea vitendo vya ukatili wa kijinsia kama vile ukeketaji na wanadai kutengwa kutumia huduma za kijamii katika maeneo hayo," amedai.

Amesema zipo baadhi ya mila potofu zinazotekelezwa na baadhi ya watu wilayani humo ikiwamo kuzuia kuolewa watoto wa kike ambao hawajafanyiwa ukeketaji wakidai ni laana hali inayochangia kuongezeka vitendo hivyo.

"Lazima tushauri vijana wetu ambao hawajaingia katika ndoa kuanzia wakati huu wakubaliane kwamba waoe wasichana ambao hawajakeketwa kama hatua kuu ya kutokomeza ukeketaji,” amesema.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya kipolisi Sirari, Chausiku Masasi, amewataka wachungaji wote ambao wanadai kutishiwa wafike katika vituo vya polisi karibu yao na kuripoti watu hao wanaodaiwa kuwatishia ili uchunguzi ufanyike.

"Kila Mtanzania ana haki sawa mbele ya sheria na hakuna nafasi ya kutekeleza vitisho wala ubaguzi wa aina yoyote kwa kuwa matendo hayo ni kinyume na sheria za nchi, kila mmoja aliyeathiriwa afike haraka polisi ili hatua sahihi zichukuliwe," amesema Chausiku.

Kila baada ya miaka miwili baadhi ya jamii wilayani hapa inadaiwa kuwaondoa watoto wao wa kike shuleni ili kuwafanyia ukeketaji na wengi kati yao wanaolewa katika umri mdogo.

Mkuu wa dawati la jinsia katika Kituo cha Polisi Sirari, Neema amesema baadhi ya wasichana wanaogopa kutoa taarifa za ukatili wa kijinsia kama vile ukeketaji kutokana na kuogopa vitisho vya baadhi ya walezi na wazazi.

"Tumeandaa utaratibu ambapo waathirika wote wanaofika kituoni hapo hupokewa na taarifa zao kuchukuliwa kwa siri kwa ajili ya kulinda faragha yao na kuonya walezi na wazazi wao kuwaadhibu bila sababu za msingi," amesema.

Miongoni mwa njia zinazotumiwa na baadhi ya wazazi wasio waaminifu kukwepa mkono wa sheria ni kuwapeleka wasichana hao kwa Ngariba nyakati za usiku ili kukwepa kuonekana.

"Wakati mwingine wanavuka mpaka na kuingia nchi jirani ambako kuna sheria dhaifu za kupinga ukatili wa kijinsia ambapo mamia ya wasichana hao kufanyiwa ukatili huo," amesema Mchungaji John.