MEWATA waombwa kutoa elimu ya ukatili wa kijinsia

By Imani Nathaniel , Nipashe Jumapili
Published at 03:52 PM Apr 21 2024
Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Ulemavu, Dorothy Gwajima, akizungumza katika Mkutano wa 36 wa chama cha wanawake Madaktari (MEWATA) uliofanyika jijini Dar es Salaam.
PICHA: IMANI NATHANIEL
Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wanawake na wenye Ulemavu, Dorothy Gwajima, akizungumza katika Mkutano wa 36 wa chama cha wanawake Madaktari (MEWATA) uliofanyika jijini Dar es Salaam.

WAZIRI wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na wenye mahitaji maalumu, Dk. Dorothy Gwajima, ametoa rai kwa wadau wa Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA), kutoa elimu kwa jamii juu ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Akizungumza jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa mkutano mkuu wa 21 wa MEWATA, unaofanyika kila mwaka, Dk. Gwajima, amesema kuwa jambo la muhimu hivi sasa ni kuwafikia wananchi hususani vijijini ambapo idadi kubwa inaonyesha kuwa wengi wao hawapati elimu ya ukatili wa kijinsia.

Amesema zipo baadhi ya sehemu hapa Tanzania bado wanaendelea kuwakeketa watoto wakike bila kujali changamoto wanayoweza kuwapata mabinti hao na kumsababisha kupoteza uhai na hata kukatisha ndoto za maisha yao.

"MEWATA jukumu lenu kubwa ni kuangalia namna gani ya kuweza kuifikia jamii kwa kutoa elimu mbalimbali kuhusu ukatili wa kijinsia, lakini niwaombe kuendelea kutoa ushirikiano serikalini kuwaza kusaidia suala afya ya mama na watoto inakuwa salama wakati wote." Amesema Gwajima.

Kwa upande wa Makamu wa Rais wa Chama cha Madaktari wanawake, Dk. Mary Sando, amesema kuwa ni vema tuendelee kuwa na mifumo ya kifikra itakayosaidia kutatua changamoto zinazojitokeza katika jamii, wapo ambao wanauana na ndoa kuvunjika lakini mila kandamizi, ukeketaji kwa watoto bado upo hapa nchini, MEWATA ni jukumu lenu kuangalia namna nzuri ya kuifikia jamii na kuitoa elimu.