Maswali magumu Askofu kujinyonga

By Peter Mkwavila , Nipashe Jumapili
Published at 11:18 AM May 19 2024
Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania, Joseph Bundala.
Picha: Maktaba
Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania, Joseph Bundala.

KIFO cha Askofu Mkuu wa Kanisa la Methodist Tanzania, Joseph Bundala, kilichotokana na kujinyonga kimeibua maswali magumu na mshangao kwa jamii kutokana na kitendo hicho kuwa kigeni ndani ya jamii.

Wakati maswali hayo yakionekana kukosa majibu, baadhi ya viongozi wa dini wameibuka na kulaani kitendo hicho kuwa ni kinyume cha maandiko matakatifu, hususan katika ukristo. 

Kutokana na nafasi ya kiongozi huyo wa kanisa kuchukua uamuzi huo, miongoni mwa maswali ni je, maziko yake yatakuwa katika itifaki na utaratibu wa Kikristo? Hiyo inatokana na hali iliyozoeleka kwamba Mkristo akijiua au kujinyonga anazikwa bila ibada, hivyo swali linaibuka kama ibada na itifaki za maziko kwa kiongozi wa dini zitafanyika. 

Askofu au mchungaji katika madhehebu ya Kikristo anapofariki dunia, maziko yake hufanyika kwa ibada maalum ambayo hujumuisha maaskofu au wachungaji kulingana na wadhifa au hadhi yake. Ibada hiyo pia huendana na maaskofu au wachungaji kusoma maneno kutoka katika Biblia Takatifu. 

Swali lingine ni kwa nini achukue hatua kama hiyo kwa sababu alizozitaja ilhali kwa nafasi yake amekuwa akikutana na watu wenye matatizo na migogoro na kuisuluhisha.   

Aidha, akiwa Askofu Mkuu ina maana kwamba chini yake kuna maaskofu katika maeneo mengine ambao angeweza kuwashirikisha na kumsaidia kuondokana na matatizo yaliyokuwa yakimkabili nani kwa nini hakufanya hivyo mpaka kuamua kujiua kwa kujinyonga. 

VIONGOZI WA DINI 

Katibu Mkuu wa Kanisa la Pentecoste Holiness Association Mission Tanzania, Askofu Julius Bundala, akizungumza na Nipashe kuhusu tukio hilo jijini hapa, amesema kitendo cha kiongozi huyo wa dini kujinyonga, kimeidhalilisha dini, serikali na jamii kwa ujumla. 

Askofu Bundala amesema kiongozi huyo alikuwa akiaminiwa na kanisa, waumini na serikali, hivyo kitendo cha kujinyonga kwake hakikubaliki kwa kiongozi mkubwa kama yeye.

“Pia hata kwa kanisa lake ambalo alikuwa akiliongoza, waumini watakuwa na mashaka. Hata viongozi wengine waliobaki na pia itakuwa vigumu kushawishi kwa watu wengi wenye kutaka kujinyonga kuwashauri wasifanye hivyo,” amesisitiza.

Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Morogoro, Jacol Memeo Ole Paulo, amesema suala hilo halijazoeleka kwa viongozi wa dini kuchukua uamuzi wa kujiua au kujinyonga.

Hata hivyo, amesema viongozi wa dini ni binadamu na si malaika, hivyo wasiposimama katika maombi na kujikita katika neno la Mungu, ni rahisi kuingia katika majaribu na hata kuchukua uamuzi kama huo. 

“Maaskofu na wachungaji wana kazi kubwa na wanakutana na mengi. Jambo la muhimu ni kusimama katika imani na kumwomba Mungu tu ili akushindie,” amesema.

Mchungaji wa KKKT na mwanataaluma, Dk. Enock Mlyuka, amesema kitendo hicho cha Askofu kuchukua uamuzi wa kujinyonga na kukatisha uhai, kimeishtua jamii na kanisa kwa ujumla. 

“Ni vigumu kuamini lakini imetokea. Katika kanisa jambo hilo ni geni kwa Askofu kujinyonga. Kwa kweli jambo hili limeliweka kanisa katika njia panda,” amesema.    

 Naye Mwenyekiti wa viongozi wa dini na madhehebu ya mkoa wa Dodoma na Kamati ya Amani, Sheikh wa Mkoa wa Dodoma, Mustaph Rajabu, amesema kujinyonga si haki kwa mwanadamu yoyote.

“Kitendo alichokifanya Askofu huyo ni sawa na kujiua mwenyewe na Mungu hahusiki na kifo hicho,” amesema.

Sheikh Rajabu amesema kuwa uamuzi aliouchukua kuna hatari ya kulisambaratisha kanisa pamoja na waumini kwa kuwa watakosa imani na viongozi wao hata kama watakuwa wakihubiri ubaya wa kujinyonga.

"Kama ni madeni hata serikali inadaiwa. Iweje  yeye aamue kujinyonga kwa kuhofia madeni hayo. Mimi  kama kiongozi kitendo alichokifanya si mpango wa Mungu bali ni shetani alimzidi kete," amesema Sheikh Rajabu. 

Naye Mwenyekiti wa Umoja wa Madhehebu ya Kikristo Mkoa wa Dodoma, Askofu Anthony Mlyashimba, alisema kiongozi huyo amekengeuka kiimani kutokana na kitendo cha kujiua mwenyewe.

“Ukizingatia kuwa maandiko yanakataza kujinyonga tena wanaofanya hivyo mbinguni hawataingia,” amesema.

Askofu Mlyashimba amesema kuwa kiongozi huyo alikuwa akitegemewa na kanisa, familia pamoja na serikali. Ni  imani yake kwa viongozi wengine waliobaki wataendelea kuhubiri matendo mema ikiwa ni pamoja na kukataza hatua za kujidhuru na ubaya wa ukatili.

Askofu Mkuu Bundala (55), alikutwa amejinyonga kwa kamba ndani ya ofisi yake iliyoko kwenye kanisani hilo, Mtaa wa Meriwa, jijini hapa huku akiacha waraka mrefu ukieleza sababu za kuchukua uamuzi huo kuwa ni madeni na mgogoro ulioko katika uendeshaji wa shule binafsi.

Bundala ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Kanisa hilo kwa Afrika, mwili wake uligundulika Alhamisi saa 1:00 usiku ukiwa unaning’inia ofisini kwake.