Kifo cha Mtangazaji Gardner Habash chawaliza wengi

By Romana Mallya , Nipashe Jumapili
Published at 10:44 AM Apr 21 2024
MTANGAZAJI nguli wa kipindi cha Jahazi, Kituo cha Redio cha Clouds FM, Gardner G. Habash.
PICHA: MAKTABA
MTANGAZAJI nguli wa kipindi cha Jahazi, Kituo cha Redio cha Clouds FM, Gardner G. Habash.

MTANGAZAJI nguli wa kipindi cha Jahazi, Kituo cha Redio cha Clouds FM, Gardner G. Habash, maarufu Captain amefariki dunia jana asubuhi katika Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), wakati akiendelea na matibabu.

Msemaji wa Kampuni ya Clouds Media Group, Emilian Mallya, amesema msiba upo nyumbani kwa marehemu maeneo ya Kijitonyama karibu na Kituo cha Polisi Mabatini.

Gargner alijipatia umaarufu mkubwa kutokana na ucheshi na aina ya utangazaji wake katika kipindi cha Jahazi na hadi umauti unamkuta, mtangazaji huyo alikuwa amelazwa katika Taasisi hiyo kutokana na maradhi ya shinikizo la damu.

Katika mahojiano yake na kipindi cha XXL yaliyofanyika mwanzoni mwa mwezi huu, Gardner alisema alianza kujisikia vibaya wiki chache zilizopita baadaye akapelekwa hospitalini ambako aligundulika kuwa na shida ambayo ililazimika kulazwa.

Machi 17, mwaka huu, binti yake ambaye ni msanii wa Bongo Flava, Malkia Karen, alitupia picha katika ukurasa wake wa Instagram akiwa na baba yake (Gardner) na mtoto wake (mjukuu wa mtangazaji huyo), wakiwa katika moja ya hoteli akimtakia kheri ya siku yake ya kuzaliwa akitimiza miaka 50.

Baadhi ya watu maarufu wakiwamo viongozi wa serikali, wanasiasa na wasanii, muda mfupi baada ya taarifa hiyo, katika kurasa zao waliweka picha ya mtangazaji huyo akiwa kazini enzi za uhai wake kama sehemu ya kuomboleza kifo chake.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, katika ukurasa wake wa Instagram ameandika, “Nimeshtushwa. Nimeumia na nimesikitishwa sana na kifo cha kaka Gardner G. Habash, mtangazaji mwandamizi wa vyombo vya habari Clouds.

“Lala salama bro (kaka), umefanya mengi katika tasnia yetu ya habari. Mwendo umeumaliza, huna baya. Poleni wanafamilia, Clouds Media, ndugu, jamaa na marafiki.”

Aliyewahi kuwa Mbunge wa Mikumi (CHADEMA), Joseph Haule na msanii wa Hip Hop, Profesa Jay ameandika, “Pumzika kwa amani ndugu yangu Captain, tangulia na sisi tunafuatia kaka.

“Poleni sana Malkia Karen, Clouds Media Group pamoja na ndugu, jamaa na marafiki cha msingi, tumuombee ndugu yetu alale salama.”

Msanii wa Bongo Flava, Nandy ameandika, “Daah! Kaka yangu pumzika kwa amani wewe ni moja ya mtu poa sana support (msaada) yako itaishi mioyoni mwetu. Rest in peace brother (pumzika kwa amani kaka).”

Zamaradi Mketema katika ukurasa wake wa Instagram ameandika, “Aaah Gadna jamani, Inalillahi waina Ilaihi Rajiun. Mungu akupumpishe kwa amani kaka, Dah! Pumzika kwa amani kaka. Kazi ya Mungu haina makosa.”

Ameanzia Kituo cha Redio cha Clouds DM, akaenda Times FM na kisha kurejea Clouds FM hadi umauti unamkuta, Gardner pumzika kwa amani.