Jaji: Hii ndiyo hatari ya kutoandika wosia

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 12:18 PM May 19 2024
Jaji wa Mahakama Kuu  Iringa, Ilvin Mugeta.
Picha: Mwandishi Wetu
Jaji wa Mahakama Kuu Iringa, Ilvin Mugeta.

JAJI wa Mahakama Kuu - Iringa, Ilvin Mugeta ameonya kuwa ni hatari kutoandika wosia, akishauri kila mwenye mali kuandika ili kuwalinda warithi wake.

Jaji Mugeta ametoa angalizo hilo wakati akiwasilisha mada juu ya Wosia na Mirathi wakati wa semina ya uwekezaji na elimu ya fedha iliyoandaliwa na Benki ya CRDB kwa wanahisa wake na Watanzania kuelekea Mkutano Mkuu wa 29 wa Wanahisa wa benki hiyo uliofanyika jana katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha (AICC), jijini Arusha. Ifuatayo ni sehemu ya wasilisho hilo:

Kifo ni jambo la uhakika kwa kila kiumbe chenye uhai. Sayansi na vitabu vya dini vimethibitisha. Biblia katika kitabu cha Mwanzo 3:19 inasema, "kwa jasho la uso wako utakula chakula, hata utakapoirudia ardhi, ambayo katika hiyo ulitwaliwa; kwa maana u mavumbi wewe, nawe mavumbini utarudi." Quran katika Surat Imran 3:185 inasema, "kila nafsi itaonja umauti. Na bila shaka mtapewa ujira wenu kamili siku ya kiama.

Baada ya KIFO, nyuma hubaki MALI zinazopaswa kurithiwa. Magonjwa, uzee, ajali na vyanzo vingine vya kifo vimempa mwanadamu uhakika, ufahamu na uzoefu mkubwa wa uwapo wa kifo. Vimethibitisha kuwa:

Kuna alama za kifo: Vyumba vya kuhifadhi maiti, makaburi ya umma na majumbani. Vyote vinamkumbusha mwanadamu hai ajiandae kimwili na kiroho!

Muda wa kufa haujulikani lakini utafika. Pengine umekaribia kufika au bado uko mbali (miaka 70) ambapo wengi hawafiki.

MAANDALIZI

Kiroho - maisha baada ya kifo (peponi na jehanamu). Kwa wanaoamini kiama. Kimwili – mali zake zitakavyotumika au kugawanywa baada ya kifo (uhusiano wa kifo na mali). Baada ya kifo ungependa mali zako zitumikeje?

Weka utaratibu wa kufuatwa kwa ajili hiyo baada ya kifo chako. Changamoto iliyopo ni kwamba wenye afya wanadhani kuwazia kifo ni jukumu la walio katika hatari ya kifo.

SABABU KUTOJIANDAA

Sababu za kutowaza juu ya kifo ni nyingi. Mathew Hale, Jaji Mkuu wa Uingereza (1609-1976) anaeleza sababu tatu: Kifo ni jambo lisilokubalika. Kuwaza juu ya kifo kunasababisha usiifurahie leo yako; kuwaza na kupanga juu ya kifo ni uchuro. Ajabu ni kwamba hata wasiowaza hufa; na ni mzima sasa, kwanini uwaze juu ya uwezekano wa kuumwa au kufa kesho? Mawazo ya kifo ni kwa wazee.

Ukweli wa mambo ni kwamba, kutojiandaa ni upuuzi. Kutafakari juu ya kifo ni faida: Unajifunza kuishi vyema katika jamii na utaandaa WOSIA bila kuchelewa na mali zako hazitapotea.

MADHARA KUTOJIANDAA

Kuna madhara makubwa usipojiandaa. Ushahidi ni mali zilizopotea. Takwimu za gawio zilizokosa wa kuzirithi katika benki ya CRDB.

Mwaka                Idadi wanahisa                Fedha (Sh.)  
 2003                         2,492                        36,882,223
 2004                         2,269                        41,346,760
 2005                         1,464                         50,224,725
 2006                         2,427                         61,990,262
 2007                         2,129                          94,453,051
 2008                         5,891                         146,459,062

Hii ina maana kwamba jumla ya Sh. milioni 431.296 zimekosa warithi baada ya wanahisa wa CRDB kufariki dunia, hivyo kupelekwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa mujibu wa sheria kutokana na wanahisa hao kutoandika WOSIA.

 TAKWIMU KORTINI

Takwimu za mahakamani zinaonesha ni asilimia tatu pekee ya kesi mahakamani ndizo zina wosia: Asilimia 80 ya kesi Mahakama Kuu hazina wosia; asilimia 90 ya kesi mahakama za wilaya hakuna wosia na asilimia 99.9 ya kesi katika mahakama za mwanzo hakuna wosia.

Takwimu hizi ni kiashiria cha kutojali: Mwislamu mwenye mtoto nje ya ndoa zingatia mirathi isizidi theluthi moja ya mali yote. Mkristo mwenye mtoto nje ya ndoa zingatia pia.

VISA MAHAKAMANI

Kuna mifano halisi ya visa mahakamani: Watoto ambao hivi sasa ni watu wazima wanataka nyumba ya baba iuzwe wagawane na mke wa marehemu; mke na watoto wameuawa ili ndugu warithi mali; watoto wa kike wamenyimwa urithi kwa kuzingatia mila za marehemu: na dada anasimamia mirathi, anauza mali na kula. Nyaraka za kufungulia kesi ameghushi na wadhamini wanakana kutia saini nyaraka za kufungulia kesi.

Ushauri wangu: Epusha usumbufu kwa wapendwa wako kwa kuandika wosia. Mafao si sehemu ya mirathi - weka kumbukumbu zako sawa kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii. 

MIRATHI

Ni mchakato wa kisheria wa kusimamia mali za marehemu ziweze kuwafikia warithi wake. Mirathi ipo ya aina mbili ambazo ni mirathi ya wosia na mirathi isiyokuwa na wosia. Sheria inayohusika katika mirathi ya mtu ndiyo huamua.

Wosia ni maandishi aliyoacha marehemu, akieleza: Mali zake, mtu wa kuzisimamia atakapofariki dunia (mtekeleza wosia), orodha ya warithi wake na mgawanyo wa mali hizo kwa warithi.

Kwa kuacha wosia, mwenye mali anakuwa na hakika utashi wake utasimamiwa, mali zake zitatambulika na kuwafikia warithi bila upotevu (fedha za gawio). Mali zikikosa warithi zinakuwa mali ya serikali.

MIRATHI YA WOSIA

Taratibu za kufungua mirathi yenye wosia ni rahisi kwa vile wosia unataja msimamizi. Mahakamani hoja ni kuthibitisha tu kama kweli wosia uliandikwa kwa viapo vya wale walioshuhudia wosia.

Hakuna haja ya vikao vya wanandugu kuteua mtu anayekubalika kwa warithi wote.

UDHIBITI WENYE TAMAA

Ugawaji umerahishwa kwani marehemu mwenyewe ndiye amegawa. Wafahamishe warithi juu ya kuwapo wosia bila kuwaeleza kilichomo.

MIRATHI BILA WOSIA

Marehemu haachi maandishi juu ya mali zake na matumizi yake. Hivyo: Utambuzi wa mali za marehemu hutegemea taarifa za watu wake wa karibu; mizozo huzuka miongoni mwa wenye sifa za kusimamia mirathi, msimamizi wa mirathi anaweza kugawa mali kinyume cha ambavyo marehemu angependa iwe. Wakishachaguliwa mamlaka yao ni makubwa sana (Bhakome), na hasara kwa uwezekano wa baadhi ya mali kutotambulika ni mkubwa. Dhuluma kwa wajane/ watoto wa kike na wenye ulemavu.

Hakuna uwezekano wa mtu kufikia mali za marehemu bila kufungua mirathi ma kuchaguliwa msimamizi au mtekelezaji wosia.

CHANGAMOTO

Kuchelewa sana kufunguliwa kwa mirathi, wanafamilia kutokuwa na taarifa kuwa marehemu alikuwa na hisa, ndugu kutokubaliana nani awe msimamizi wa mirathi na wasimamizi kutofanya majukumu yao kwa moyo na kwa uaminifu. Kuepuka haya, chagua mtu unayemwamini kwa kuandika wosia.

MAPENDEKEZO

Kila mtu anayemiliki mali anapaswa kuandika wosia ili kuwalinda warithi. Wadau wa sekta ya benki washirikiane na mahakama na Ofisi ya Kabidhi Wasii kutoa elimu kwa umma kuhusu wosia, taratibu na faida zake.

Jielimishe kuhusu taratibu za mirathi na uliyepata elimu hii, chukua hatua sasa na mfahamishe na mwenzako. Mali tunazochuma hatuzikwi nazo baada ya kifo.

Mwenye mali akifa bila kuweka utaratibu wa upatikanaji na matumizi ya mali zake zinaweza kupotea au kutumika kinyume cha ambavyo angependa yeye zitumike.

Kuandika wosia ni hekima na ustaarabu kwani siku ya kifo haifahamiki. Wosia huepusha mafarakano katika familia. Kutoandika wosia ni hasara kwa marehemu na kwa wapendwa wake.