Ajali ya boti yaua watu 58 Afrika ya Kati

By Mwandishi Wetu , Nipashe Jumapili
Published at 01:41 PM Apr 21 2024
Juhudi za uokoaji kwenye mkasa wa kuzama kwa boti nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.
Picha: JeffersonCF/Xinhua/picture alliance
Juhudi za uokoaji kwenye mkasa wa kuzama kwa boti nchini Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

TAKRIBANI watu 58 wamefariki dunia katika ajali ya boti nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, baada ya boti hiyo kupinduka na kuvunjika vipande muda mfupi baada ta kung’oa nanga kwenye Mto Mpoko uliopo karibu na mji mkuu wa Bangui.

Maafisa wameviambia vyombo vya habari nchini humo kuwa wanawake wengi na watoto ni miongoni mwa waliofariki katika ajali hiyo.

Kwa mujibu wa ripoti za Idara ya kushughulikia majanga, wafanyakazi wa uokozi waliwasili katika eneo la ajali dakika 40 baada ya boti hiyo kuzama. Abiria 300 walikuwa wakielekea kwenye mazishi huku watu kadhaa wakiwa bado hawajulikani walipo.

Serikali haikuzungumzia tukio hilo lakini katika hotuba iliyorekodiwa na kurushwa hewani siku moja baadae, msemaji wa serikali Maxime Balalou aliripoti kuwa idadi ya awali ya vifo ilikuwa watu 30.

Serikali imetangaza kuanzisha uchunguzi na kuweka utaratibu wa kuzisaidia familia za waathirika. Usafiri wa majini hutumika zaidi katika Jamhuri ya Afrika ya Kati kwa sababu barabara nyingi ziko katika hali mbovu. Lakini boti nyingi zimetengenezwa kwa mbao na hazitunzwi vizuri.

DW