Nchimbi: Changamikieni mikopo 10%, puuzeni maandamano

By Halfani Chusi , Nipashe Jumapili
Published at 12:34 PM Apr 21 2024
Katibu Mkuu CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.
PICHA: MAKTABA
Katibu Mkuu CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka wananchi kupuuza maandamano yanayoandaliwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), badala yake watumie muda wao kwenda kuchukua mikopo ya asilimia 10 iliyorejeshwa na serikali.

Katibu Mkuu CCM, Balozi Dk. Emmanuel Nchimbi, ametoa kauli hiyo wakati akihutubia wananchi mkoani Njombe na kuonya baadhi ya viongozi wa CCM kuwa madalali kwa wanaotaka kuwa viongozi na kusisitiza tabia hiyo itafarakanisha chama. 

Amesema kazi kubwa iliyofanywa na serikali ndani ya miaka mitatu ni nyenzo inayobeba ukweli wa kutosha kusambaratisha uongo unaoenezwa na baadhi ya wapinzani wa kisiasa kupitia mikusanyiko yao. 

Balozi Nchimbi amewataka wanaCCM wote kuendelea kujiamini na kutembea kifua mbele wanapozisema, kuzitangaza na kuikumbusha jamii kuhusu kazi za maendeleo na ustawi wa jamii, zinazofanywa na serikali  ili wananchi waendelee kuona ukweli, wakitofautisha na uongo unaoenezwa kwa propaganda nyepesi za kisiasa. 

“Mambo yaliyofanywa na serikali ndani ya miaka mitatu, unaweza kuona kama ni miujiza, kazi kubwa sana inafanyika ni wajibu wetu kuyatumia mazuri hayo kukipambania chama,” ameagiza.

Ameliwasisitiza watendaji wa chama na serikali ulazima na umuhimu wa kuwa waadilifu wakati wote kwenye masuala yanayohusu rasilimali za umma, kwa kupiga vita rushwa na ubadhirifu.

Pia, amewataka wananchi kulinda miradi inayotekelezwa na serikali akiwataka kuitunza kwa wivu mkubwa na uzalendo.

“Serikali ya CCM inatekeleza miradi mingi na inatumia fedha nyingi za umma, lazima viongozi wahakikishe fedha zile hazipotei zinatumika kulingana na maelekezo ya serikali.

“Viongozi wa dini na wa kimila endeleeni kusisitiza uadilifu ndani ya nyumba na nje ya nyumba zetu ili tujenge chama imara, lazima wana-CCM tuwe na umoja. Simamieni haki bila kubaguana kwa itikadi za siasa, dini, na ukabila.

“Tufanye kazi ya kutangaza mazuri ya CCM, kwa miaka mitatu kazi iliyofanyika Njombe ni kama miujiza. Kuna wakati watu wanasahau mazuri yaliyofanywa na serikali. Kuna watu watazunguka huko watasema, chama hakijafanya lolote, mtu wa aina hiyo mpuuzeni, lakini mpingeni kwa hoja.”

Kupitia mkutano huo, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Anthony Mtaka, amewasilisha taarifa ya mrejesho wa utekelezaji wa Ilani ya CCM ya 2020-2025, iliyohusisha miradi mbalimbali ya maendeleo na ustawi wa wananchi.

Katika ziara yake, Balozi Nchimbi wakati akielekea Songea, amepitia Wilaya ya Madaba, mkoani Ruvuma na kusalimia wananchi wa eneo hilo na kuwaahidi serikali itaendelea kununua mazao kwa wakulima ili kuwaepusha na wafanyabiashara wanyonyaji.

Katika ziara hiyo, Nchimbi ameambatana na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Amosi Makalla na Katibu wa Oganaizesheni, Issa Gavu.