Mvua yapunguza kasi upigaji kura

By Waandishi Wetu , Nipashe
Published at 10:24 AM Nov 28 2024
Foleni ya kupiga kura.
Picha: Mpigapicha Wetu
Foleni ya kupiga kura.

KATIKA baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa mvua iliyoanza kunyesha kuanzia majira ya saa 12:00 asubuhi hadi saa 6:30 mchana ilipunguza kasi ya upigaji kura kutokana na baadhi ya vituo watu kwenda mmoja mmoja tofauti na utaratibu wa kawaida wa kuwa na mistari.

Hadi mvua inakata mwandishi wa habari hii alishuhudia wapigakura wasiopungua 10 walioingia kituoni hapo.

Baadhi ya wapigakura waliofika kwa ajili ya kutekeleza haki yao ya kupiga kura akiwamo mkazi wa Majengo, Elizabeth Popa akizungumza na Nipashe baada ya kupiga kura alisema hakupata usumbufu wowote licha ya kuwa hali ya hewa kuwa ya mvua na kusababisha msongamano kutokuwa mkubwa.

“Mimi nimefika sasa hivi sijakuta foleni na nimepiga kura bila usumbufu nimeona jina langu na sasa naenda kwenye majukumu yangu," alisema Popa.

Naye Dotto Mathias alisema uchaguzi huu umefanyika kwa uhuru na haki na wasimamizi wanatoa maelekezo na unapiga kura bila kubugudhiwa hali ikiendelea hivyo mpaka jioni hatutakuwa na machafuko yoyote.

Kwa mujibu wa msimamizi wa kituo cha kupigia kura kilichopo Kata ya Bukandwe, Kijiji cha Ihayabuyaga, Magu, Mwanza, Valery Shigi, hadi kufikia majira ya saa sita walijitokeza wapiga kura wasiozidi 100. 

Mkazi wa Mtaa wa Pwani, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Aline Ngw'aganugu, alisema, licha ya kuwa na mvua, ameweza kutoka ndani ili kutimiza haki ya kikatiba ya kuchagua kiongozi ambaye atakuwa msaada na mpigania wananchi wake.

Alisema katika kituo ambacho amepigia kura majina ya wapigakura yameonekana licha ya kuwa sio mengi zaidi sawa na vituo jirani ambavyo vina idadi kubwa ya wapigakura.

Mkazi wa Kahololo, Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera, Joseph Alphonce, alisema katika ubao wa matangazo namba ya jina lake inatofautiana na iliyopo ndani katika jina la pili hali iliyosababisha utata awali, lakini baadaye akapiga kura na kuendelea na shughuli zake.

Mkazi wa Mtaa wa Uwanja wa Ndege wilayani Maswa, Simiyu, Phaustine Makeja, alisema kulikuwa na utaratibu mzuri na kuwa wasimamizi walikuwa wakisaidia kufanyika haraka licha ya mvua kunyesha, lakini hawakukutana na usumbufu wowote.

Diwani wa Kata ya Bukandwe, Marco Minzi, alisema wananchi wamejitokeza kwa wingi kuwapigia kura viongozi wao wanaowahitaji licha ya kuwapo na mvua zilizoanza kunyesha alfajiri hadi saa sita mchana huku akiwasihi wananchi kuendelea kujitokeza kupiga kura. 

VIONGOZI WANENA 

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, akizungumza wakati wa kupiga kura katika Kituo cha Isamilo jijini Mwanza baada ya kubaini upungufu wa wapigakura aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura bila kujali mvua inayoendelea kunyesha.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa, akizungumza baada ya kupiga kura kwenye kituo cha Pwani kilichopo Manispaa ya Bukoba mkoani humo aliwataka wananchi kuendelea kupiga kura kwa utulivu ili kukamilisha uchaguzi bila kuwapo kwa vurugu. 

Alisema mkoa huo uko salama na wananchi wanaendelea kujitokeza kwa wingi katika vituo vyao kutimiza haki ya kupiga kura huku akiwaomba wananchi kuwa watulivu na kuzingatia taratibu za kupiga kura na wakimaliza warudi nyumbani kwao wapumzike wasubiri matokeo na asiwepo wakujaribu kufanya vurugu. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Anamringi Macha, alisema uchaguzi mkoani humo umefanyika kwa amani na utulivu, hakuna vurugu zozote kubwa ambazo zimefanyika za kuvuruga amani ya nchi. 

Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Mbunge wa Jimbo la Maswa Mashariki, Stanslaus Nyongo, alisema upigaji kura unafanyika vyema na kuwa wananchi wameendelea kujitokeza kupiga kura na kuelekezwa cha kufanya pale wanapokwama hivyo kuwataka wasimamizi wa uchaguzi kuhakikisha wanaendelea kutoa ushirikiano ipasavyo kwa wapiga kura hao. 

WAKOSA MAJINA VITUONI

Baadhi ya wananchi Joseph Peter Mkazi wa Manispaa ya Shinyanga wamelalamikia hatua ya kutobandikwa majina yao kwenye vituo vya kupigia kura, huku wengine wakidai kutoyaona  na hivyo kushindwa kupiga kura.

Peter alisema katika kituo cha kupigia kura soko la Ndala Manispaa ya Shinyanga, alisema orodha ya majina ya wapigakura haikubandikwa kituoni hapo, hali ambayo iliwapa changamoto ya kuhakiki majina na hata kusababisha foleni kuwa ndefu. 

Naye Katibu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Serengeti, Jackson Mnyawami, alikiri kuwapo kwa tatizo hilo na kuwa baadhi ya vituo ambavyo amevitembelea orodha ya majina ya wapigakura hayajabandikwa, na hivyo kusababisha usumbufu kwa wananchi.

 Estormine Henry, mkazi wa Mtaa wa Bugweto, alisema katika kituo chake cha kupigia kura hakuona jina lake, na kuamua kuondoka na kushindwa kupiga kura.

Mkazi wa wilayani Kahama, Zaria Kilimba alisema, licha ya kushiriki kikamilifu na kupata jina lake awali, lakini jana wakati wa kupiga kura alikosa jina hilo na kuondoka bila kupiga kura.

Msimamizi wa uchaguzi katika Manispaa ya Shinyanga, Alexius Kagunze, akizungumzia suala la majina ya wananchi kutobandikwa kwenye baadhi ya vituo vya kupigia kura, alisema, kwenye vituo vya wazi ambavyo vipo 149 majina hayo hayajabandikwa kutokana na kuhofia mvua kulowesha makaratasi.

Alisema katika vituo hivyo vya wazi walichokifanya, daftari lenye orodha ya majina ya wapigakura, lilikuwa kwa wasimamizi wa uchaguzi kituoni na kila mtu kuhakikiwa jina lake na kushiriki kupiga kura. 

Nipashe ilifanikiwa kuongea na baadhi ya wasimamizi wa vituo vya Nyasho Kati, Sido na Nyamatare, ambao walisema wananchi waliokosa majina yao kwenye ukuta wameyakuta kwenye daftari la kudumu la wapigakura na kuendelea kupiga kura. 

MGOMBEA MMOJA 

Mkazi wa wilayani Magu mkoani Mwanza, Emmanuel Mashauri, alisema hakwenda kupiga kura kutokana na eneo lake kuwa na mgombea mmoja na kuwa haoni haja ya kujisumbua kushinda kwenye kituo cha kupiga kura ili hali tayari mshindi anajulikana.

Naye Hawa Ramadhani Mkazi wa Mtaa wa Rwagasole jijini Mwanza alisema kuenguliwa kwa wagombea ambako kulileta sintofahamu kwa wananchi kumesababisha kutokuwa na hamasa ya kushiriki uchaguzi huo na kuamua kuendelea na shughuli za kibiashara. 

KAMPENI VITUONI 

Wananchi wa Kata ya Nyakato Mtaa wa Baruti, Kituo cha Sido Manispaa ya Musoma mkoani Mara, walilalamikia baadhi ya  mawakala na wanachama  wa vyama vya siasa kufanya kampeni za siri ndani ya vyumba vya kupigia kura wakiwalazimisha kupiga kura kwa vyama vyao. 

Mpigakura Musira Aloyce alisema kuwa baadhi ya mawakala na wanachama kuwaelekeza wananchi kuchagua chama fulani bila wao kujua kuwa anayemhamasisha ni wa chama gani.

Uchunguzi uliofanywa na mwandishi wa gazeti hili ulibaini kuwapo kwa orodha ya majina yaliyobandikwa katika mbao za matangazo huku namba za majina zikiwa zimefunikwa na kusababisha wapigakura kuondoka bila kupiga kura na baadhi yao kuoneshwa majina yao kwenye daftari na kuelekezwa kuchagua chama.

Aidha, hali hii ilimfanya Mgombe wa nafasi ya ujumbe kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Mtaa wa Nyahanga, Amri Mambo Kiboge, kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa muda baada ya kuonekana anapinga watu kuelekezwa namna ya kupiga kura huku wakiwa wanajua kusoma na kuandikwa.

Alisema, alitakiwa kuwekwa ndani kwa muda wa wiki mbili baada ya kutolewa amri na msimamizi wa uchaguzi, lakini amekuja kuachiwa mbele ya viongozi wake wa chama wilaya, kimkoa na kikanda waliopo kituo cha polisi Kahama.

Msimamizi wa uchaguzi wa mtaa wa Nyahanga, Elleni Mugenyi, alikiri baadhi ya wapigakura kukosa majina yako kwenye mbao za matangazo lakini kwenye daftari yalipatikana na kuhusu mgombea wa Chadema kukamatwa ni kweli kwasababu alikuwa kwenye chumba huku akiwa tayari ameshapiga kura.

Katibu Mwenezi wa CHADEMA Wilaya ya Kahama mkoani Shianyanga, Mustafa Kiyege, anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa tuhuma za kufanya vurugu kwenye kituo cha kupiga kura Mwime Machimboni wakati akizuia mawakala wa CCM aliodai kuingiza kura kwenye boksi zilizokuwa tayari zimepigwa.

Mwenyekiti wa chama hicho, Bukango Mussa aliyabainisha hayo wakati akizungumza na vyombo vya habari katika kituo cha kupiga kura cha Bukondamoyo Shuleni.

Jijini Mwanza wakati wa upigaji kura ukiendelea Msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Jiji la Mwanza ambaye pia ni Mkurugenzi wa Jiji, Kiomoni Kibamba alikiri kukamatwa kwa vijana wa Chadema Kata ya Lwanima wakidaiwa kuvamia kituo na kuondoka na karatasi za kupigia kura na kwenda nazo mahali pasipo julikana.

Imeandaliwa na Vitus Audax (MWANZA), Neema Emannuel (MAGU), Remmy Moka (MWANZA), Elizabeth Faustine (MAGU), Restuta Damian (KAGERA), Shaban Njia (KAHAMA), Marco Maduhu (SHINYANGA), Na Ada Ouko (MUSOMA).