VIGOGO wa vyama vya siasa, jana walihitimisha kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika leo kwa staili tofauti kwenye maeneo mbalimbali nchini.
Wakati kampeni hizo zikihitimishwa, Rais Samia Suluhu Hassan amewahakikishia wapigakura kuwa uamuzi wao utaheshimiwa.
Rais Samia amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa uwazi, haki na kwa kuzingatia kanuni za uchaguzi zilizoko.
Akizungumza jana na Watanzania kuhusiana na uchaguzi huo, alisema ni muhimu kuheshimu uamuzi wa wapigakura, kwa kuwa demokrasia yenye nguvu hujengwa kwa misingi ya heshima na mshikamano.
Rais aliwakumbusha viongozi wa vyama vya siasa, mawalaka na wasimamizi wa uchaguzi kuzingatia na kuheshimu sheria na kanuni za uchaguzi ili uwe wa haki. Pia aliwakumbusha wasimamizi wa uchaguzi na wote wanaohusika na mchakato huo, kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa haki, uwazi na kuzingatia taratibu zilizokubaliwa na wadau.
Aidha, alitoa rai kwa kila mdau wa uchaguzi kutoa ushirikiano ili kufanikisha adhma ya kuwa na uchaguzi wa amani unaoakisi heshima kwa taifa lenye mshikamano na demokrasia imara.
Aliwakumbusha Watanzania kuwa kupigakura ni haki yao ya msingi, hivyo jukumu lao ni kuhakikisha wanaitumia kudumisha amani na utulivu na kujiepusha na vitendo vya uchochezi, vurugu au uvunjifu wa sheria.
Rais Samia alisema ni fursa muhimu kwa kila Mtanzania mwenye sifa ya kupiga kura kuchangia maendeleo ya nchi kwa njia ya kidemokrasia kwa kuchagua kiongozi mwenye sifa huku akiwasihi kujitokeza kwa wingi kupiga kura kwa kuwa ni fursa ya kuhakikisha uamuzi unaohusisha jamii unatokana na mahitaji halisi ya wananchi.
“Serikali za mitaa ni msingi wa ujenzi wa taifa imara na lenye maendeleo endelevu, kupitia viongozi tunaowachagua tunaweka misingi thabiti ya uwajibikaji na utoaji wa huduma bora kwa wananchi na usimamizi wa rasilimali za umma,” alisema.
FUNGA KAZI
Akifunga kampeni hizo zilizofanyika viwanja vya Liwale, mkoani Lindi jana, Waziri Mkuu na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa, aliwapigia debe wagombea wa chama hicho huku akisema kimechagua majembe ili kuwaletea Watanzania maendeleo.
Katibu Mkuu wa CCM, Dk. Emmanuel Nchimbi, aliwaonya wagombea wa chama hicho watakaoshinda katika uchaguzi huo kutotumia madaraka yao kuwaumiza wananchi.
Alisema chama hakitakuwa na huruma kwa kiongozi wa namna hiyo na kwamba atachukuliwa hatua kali ikiwamo kutenguliwa. Alisema hayo jana wilayani Temeke katika Jimbo la Mbagala wakati akifunga kampeni za uchaguzi huo.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, John Mongella, akifunga kampeni hizo mkoani Shinyanga, aliwataka wananchi wa Shinyanga wachague wagombea kutoka CCM ambao ndio watawaletea maendeleo.
CHADEMA TUMEPITIA MAPITO
Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrsia na Maendeleo (CHADEMA) Bara, Tundu Lissu, alisema: “Tumepitia mapito mengi katika uchaguzi huu. “Tumehangaika sana katika rufani. Hawa wagombea tulio nao tumeshinda majaribu kwa sababu hatukukata tamaa.”
Akifunga kampeni Ikungi mkoani Singida, Lissu alisema wamepitia mapito hayo bila sababu za msingi kwa kuwa watu waliopewa dhamana ya kuusimamia, hawakusimama vizuri katika nafasi zao.
Alisema licha ya chama kusimamia wagombea wengi, zaidi ya nusu wameenguliwa kwa sababu zisizo za msingi.
ZITTO AFUNGUKA
Kiongozi mstaafu wa ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe, akifunga kampeni za chama hicho, alisema uchaguzi huo umeonesha ni kwa namna gani chama chao kimekua na kuimarika.
Alisema katika maeneo yote ambayo viongozi wakuu wa chama hicho walitawanyika, kote walisimamisha wagombea wenye nguvu na kwamba, wana uhakika wa kushinda leo.
“Mbegu mliyoipanda katika chama hiki imemea, imekua. Na imekua limtii likubwaa la Mlumba ambalo linaendelea kushamiri Jamhuri nzima ya Muungano. Watu wa Kigoma hongereni kwa kazi kubwa mliyoifanya,” alisema.
VITUO VYAONGEZWA
Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Shinyanga, Emmanuel Ntobi, amelalamikia ongezeko la vituo vya kupigia kura katika Manispaa ya Shinyanga bila wao kushirikishwa ili kuweka mawakala.
Alisema awali waliambiwa vituo vya kupigia kura vitakuwa 163, lakini jana jioni wakashtukizwa na kuambiwa vimeongezeka 122 na kufika 285, jambo ambalo wamelalamikia huenda ni maandalizi ya ‘bao la mkono’.
Katibu wa CHADEMA, Kanda ya Victoria, Zakaria Obadi, alisema vituo tisa pia vimeongezwa katika kata ya Nyegezi jijini Mwanza tofauti na idadi ya mawakala waliowaandaa.
AHAMIA CCM
Mgombea Uenyekiti wa ACT Wazalendo katika Kijiji cha Igung'wa, Kata ya Kitwana, Kahama mkoani Shinyaga, William Nkwabi, ameandika barua ya kujitoa katika nafasi hiyo na kujiunga CCM.
Mgombea wa CHADEMA katika Mtaa wa Buswelu ‘A’ wilayani Ilemela, Mwanza, Pastory Apolinary, amedaiwa kupotelea kusikojulikana baada ya kupokea simu ikimtaka kwenda kuchukua mchango wa kampeni.
Nkwabi alisema ameamua kuandika barua hiyo baada ya kupimwa na daktari na kubaini kuwa anatakiwa kupumzisha mwili wake kutokana na umri alio nao kwa sasa, hivyo hawawezi kukimbizana na kampeni.
Alisema amefikia uamuzi huo bila kushawishiwa na mtu na akiwa na akili timamu, hivyo kwa sasa atakuwa mwananchi wa kawaida na kushiriki uchaguzi wa viongozi na wajumbe wa serikali ya kijiji kama walivyo wengine.
“Nitamuunga mkono mgombea wa CCM, ninawaomba wafuasi wangu wa ACT Wazalendo kuungana nami kumuunga mkono mgombea wa CCM. Kabla ya kujiunga na ACT Wazalendo, nilikuwa CCM,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM, Kata ya Maalunga, Baraka Jilumbi alisema, mlango wa chama chao uko wazi kwa mtu yeyote anayetaka kujiunga.
Mwenyekiti wa CHADEMA Kanda ya Victoria, Hezekiah Wenje, alisema: “Ilikuwa saa 7:00 mchana mgombea wetu akijiandaa na mkutano, mtu akampigia simu akamwambia ni mdau wa CHADEMA anataka niwape mchango kidogo katika kampeni. Akaenda kuonana na huyo mtu ndipo akapotea moja kwa moja mpaka jioni alikuwa hajaonekana.”
Wenje alisema tayari taarifa imeshatolewa Jeshi la Polisi, huku wakiendelea kufuatilia mawasiliano ya mtu huyo aliyemwita.
Akizungumza kwa njia ya simu, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Naibu Kamishna (DCP) Wilbrod Mutafungwa, alikanusha kuwa na taarifa za kutekwa kwa mgombea huyo, lakini akasema wanafuatilia kujua ukweli wa madai hayo.
UVAMIZI OFISI CHADEMA
Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, amelaani na kukemea vikali tukio la ofisi za chama hicho katika Kata ya Soweto, Manispaa ya Moshi, kuvamiwa na watu wasiojulikana, kupiga viongozi waliokuwamo, kuvunja vizimba vya chama hicho, Soweto na First & Last.
Akizungumza jana na waandishi wa Habari kabla ya mkutano wa kuhitimisha kampeni, Lema alisema: “Tunawaomba polisi, warudi katika kazi yao wawafuate na wafanye upelelezi kama ambavyo wanafanyaga upelelezi kutoka kwetu.
“Vitisho vinaathiri sana ustawi wa amani na maisha ya pamoja ya kijamii. Baada ya uchaguzi bado sisi ni ndugu, bado sisi ni majirani tutatibiwa hospitali moja, tutapanda daladala zile zile baada ya uchaguzi. Hii kutishana hii si ya kisiasa tu, inaingia kwenye maisha ya kijamii.
“Wamewatisha wagombea wetu kwamba, wasipojitoa watawafanyizia na baada yake wamejitoa. Wanawatisha viongozi wetu, wengine hawataki hata kutoka nje. Sasa hivi vitisho havitaishia katika uchaguzi, vitaendelea baada ya uchaguzi. Jeshi la Polisi fuatilieni vitisho tunavyofanyiwa.”
Kwa mujibu wa Lema, kuna vitisho vimefanywa katika Kata ya Mabilioni, Halmashauri ya Wilaya ya Same, vingine vimefanywa katika Kata ya Miembeni, Mtaa wa Langoni, Manispaa ya Moshi, ambako mgombea amehama Moshi kabisa.
“Kule Soweto, Manispaa ya Moshi, nako wagombea wetu si mmoja, wametishiwa. Wale waliosimama imara ndio hili tukio la kuvamia ofisi limetokea.
“Tuna vitisho Siha, Kata ya Karansi na Kata ya Ngarenairobi. Tuna vitisho Vunjo, tuna vitisho tunavyo Rombo. Sasa kwa bahati mbaya tuna taarifa ya vitisho vingi usiku huu na kamatakamata ya vijana wa CHADEMA.
“Tunashauri kuwakamata haindoi ujasiri wa kuipenda nchi yao, hatujengi uzalengo kwa kuharibu imani ya watu kwenye nchi yao,” alisema.
VIJANA CCM
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Mohammed Kawaida, alizungumza na waandishi wa habari akisema uchaguzi huo usiwe wa kupuuza, bali iwe fursa muhimu kwa kila Mtanzania hasa vijana kuonesha dhamira ya kweli ya kuleta maendeleo endelevu kwa taifa.
Alisema Watanzania wote wana wajibu wa kuchagua viongozi waadilifu, wanaojali maslahi ya wananchi na wenye uwezo wa kusimamia maendeleo na kusisitiza kuwa ni muhimu Watanzania kuchagua viongozi ambao wanaona wanafaa katika kuleta maendeleo.
“Kuna sababu mbalimbali za msingi za kwa nini, wananchi wanapaswa kuiunga mkono CCM katika uchaguzi huu wa serikali za mitaa ikiwamo suala la kuona mafanikio ya kiuchumi.
“Mengine ni ustawi wa jamii kupitia miradi mikubwa ya kimkakati ambayo imetelezwa ikiwamo Reli ya Mwendokasi (SGR), Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere (JNHPP), na uboreshaji wa bandari yamefungua fursa nyingi za ajira na kukuza uchumi wa ndani,” alisema.
Aliongeza kuwa: “CCM ni chaguo bora kwa Watanzania kutokana na historia yake, mafanikio na sera zake zinazojikita katika ustawi wa kila raia ambako kimewezesha utoaji wa elimu bila malipo, afya, maji safi na salama, uwezeshaji wa vijana, wanawake, na wenye ulemavu huku kikitambua nafasi ya makundi yao katika maendeleo ya taifa.”
Kawaida alisema katika uchaguzi huo ni muhimu kwa wananchi kuendelea kuichagua CCM ili kuhakikisha mabadiliko hayo yanaendelea, na miradi ya maendeleo inazidi kuwa na tija kwa jamii nzima.
Alisema chama hicho kinatambua mafanikio ya serikali katika ngazi zote za kitaifa, yanategemea ufanisi wa viongozi wake na kwamba, chama kimewekeza katika kuwaandaa na kuwajengea uwezo viongozi wake kupitia mafunzo ya uongozi na utendaji.
POLISI KUSAMBAZWA
Jeshi la Polisi nchini, kupitia taarifa yake iliyotolewa jana na Msemaji wake, Naibu Kamishna wa Polisi (DCP) David Misime, ilisema wananchi wataona askari polisi mtaani, nje ya vituo vya kupigia kura.
Alisema askari polisi hao watasambazwa kwa lengo la kuhakikisha usalama unakuwapo wakati wote wa kupiga kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo.
“Jeshi la Polisi linatoa wito kwa kila Mtanzania kuhakikisha anadumisha amani, utulivu, upendo na usalama kipindi chote cha kupiga kura, kuhesabu kura na kutangaza matokeo na baada ya uchaguzi.
“Kamwe usiwe chanzo cha uvunjifu wa amani, kwani hutaonewa muhali, lazima utachukuliwa hatua za kisheria.
“Kamwe tusiwape nafasi, wala kusikiliza au kufuata matamshi na vitendo vya viongozi au wafuasi wao ambayo lengo lake ni kutaka kuvuruga amani, utulivu na usalama wa nchi yetu,” alisema Misime.
· Imeandikwa na Godfrey Mushi (MOSHI), Romana Mallya, Jenifer Gilla, Gwamaka Alipipi,Maulid Mmbaga, Elizabeth Zaya, (DAR), Shaban Njia (KAHAMA), Vitus Audax (MWANZA), Judith Julius, (NGARA) na Marco Maduhu (SHINYANGA).
© 2024 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED