MAKAMU wa pili wa Rais wa Zanzibar Hemed Suleiman Abdulla amewataka Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutowachukia wagombea wa vyama vingine waliojitokeza kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa kwani wameshiriki kukamilisha Demokrasia.
Makamu huyo wa Rais ameyasema hayo alipokuwa akifunga kampeni za Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Mkoa wa Pwani katika Viwanja vya Mailimoja Kibaha ambapo amesema kitendo cha kuwepo kwa vyama vingine kugombea kwenye uchaguzi huo kinaleta ushindani.
Amewataka wanachama wa chama hicho pamoja na wananchi kwa ujumla kwenda kuwachagua wagombea wa CCM ili waendeleze kuleta maendeleo kwenye maeneo yao.
“Hawa wa vyama vingine wamekuja tuwashinde sisi hatuna huruma kwenye uchaguzi, wala hatuna urafiki likija swala la uchaguzi tupambanie kwanza kushinda halafu baadae ndio tutashiriki kwenye kula pamoja, hata wapinzani niwaombe wasipoteze kura zao kwa mtu ambaye wanajua hatashinda wapeni kura wagombea wa CCM waendelee kuongoza na kuleta maendeleo,” amesema.
Amesema wanawake ni kundi ambalo likiamua jambo lake linatekelezeka kwa asilimia kubwa hivyo aliwaomba kujitokeza kwa wingi kwenda kuwapigia kura wagombea wa CCM
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao amesema ushindi kwa wagombea wa chama hicho ni zaidi ya asilimia 95 na kwamba wananchi wanatambua kazi nzuri iliyofanywa na Serikali hivyo wataenda kukipigia kura chama hicho.
Naye Mjumbe wa Kamati ya Uchumi (CCM) Mkoa wa Pwani na Taifa Ahmed Salum amesema kampeni za mwaka huu ni za kidigitali na wanaamini chama hicho kinakwenda kushinda kwa kishindo kutokana na mambo mazuri yaliyofanyika.
Mgombea nafasi ya Mwenyekiti mtaa wa Tangini Idd Mfaume (CCM) amesema kitendo cha wapinzani kuweka wagombea kimeleta chachu kwenye kampeni lakini wanaamini wananchi bado wana Imani na chama hicho wataenda kuwapigia kura wagombea wake.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED