Pikipiki 10, ‘ambulance’ kuboresha afya

By Marco Maduhu , Nipashe
Published at 08:21 PM Jan 02 2025
Bodaboda 10, ‘ambulance’ kuboresha afya
Picha: Marco Maduhu
Bodaboda 10, ‘ambulance’ kuboresha afya

WIZARA ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais TAMISEMI, imetoa magari manne ya wagonjwa (ambulance), likiwamo la gari la chanjo na pikipiki 10 ili kuboresha huduma za afya mkoani Shinyanga.

Vitendea kazi hivyo zimekabidhiwa Januari 2, 2025 na Katibu Tawala wa Mkoa wa Shinyanga, CP Salum Hamduni, kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo, Anamringi Macha, kwa waganga wakuu wa halmashauri na kaimu RMO.

Hamduni akizungumza katika hafla hiyo, ameipongeza serikali, kwa kuendelea kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya, kwa wananchi na kutoa vitendea kazi hivyo.

“Kwa niaba ya serikali kupitia Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI ninakabidhi magari manne ya wagonjwa, ambayo yanagawiwa katika halmashauri nne Msalala, Ushetu, Kishapu na Shinyanga DC na gari moja la mkoa, kwa ajili ya kusambaza chanjo kwenye halmashauri,” amesema Hamduni.

Tawala wa Mkoa wa Shinyanga CP Salum Hamduni (kushoto)akimkabidhi gari la kubeba wagonjwa Ambulance Mganga Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Dk. Nuru Yunge
“Pikipiki hizi 10, moja inapewa Manispaa ya Kahama na moja Shinyanga, Msalala inapewa pikipiki mbili, Shinyanga DC mbili, Kishapu mbili na Ushetu mbili. Kazi zake ni kusambaza chanjo kwa wananchi, mara baada ya gari hili la chanjo la mkoa kuzifikisha ngazi ya halmashauri,” ameongeza.

Ametoa wito kwa waganga wakuu wa halmashauri, kwamba vitendea kazi hivyo wavitunze na vitumike kwa madhumuni yaliyokusudiwa, huku akiwasihi madereva kwamba waviendeshe kwa kuzingatia sheria za usalama barabarani na atakayeharibu kwa makusudi magari hayo, serikali itamchukulia hatua.

Akizungumza kwa upande wa pikipiki za kusambaza chanjo, ameonya kwamba zisije kugeuzwa kwa matumizi ya kufanya biashara ya bodaboda, bali zisaidie wananchi kupata huduma ya chanjo.

Bodaboda 10, ‘ambulance’ kuboresha afya
Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Faustine Mlyutu, ambaye ni Mratibu wa Miundombinu ya Afya Mkoa wa Shinyanga, ameishukuru serikali kwa kuendelea kuboresha huduma za afya mkoani humo, akitoa wito kwa wananchi kwamba, wajitokeze kwa wingi kupata chanjo, ili kuimarisha afya zao na watoto.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Dk. Nuru Yunge, amesema gari la wagonjwa ambalo wamepatiwa pamoja na pikipiki mbili, zitasaidia kwa kiasi kikubwa kutoa huduma bora za afya kwa wananchi.