Dereva basi kizimbani, asomewa mashtaka 22

By Vitus Audax , Nipashe
Published at 09:57 AM Jan 04 2025
news
Picha:Mtandao
Basi la Kisire.

DEREVA wa basi la abiria la Kisire linalofanya safari zake kati ya Mwanza na Sirari mkoani Mara, Adam Charles (30), amepandishwa kizimbani na kusomewa shtaka moja lenye makosa 22 ikiwamo kusababisha majeruhi kwa abiria na uharibifu wa mali.

Charles alipandishwa kizimbani jana na kusomewa shauri hilo la usalama barabarani katika Mahakama ya Wilaya ya Magu, mkoani Mwanza mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Erick Kimaro. 

Akisoma shtaka hilo mbele ya Hakimu Kimaro, Mwendesha Mashtaka wa Serikali, Nuru Nko, alidai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa la uharibifu wa mali ambayo ni basi alilokuwa akiendesha namba T. 229 DST.

Nko alidai mahakamani hapo kuwa mshtakiwa wakati akiendesha basi la Kampuni ya Kisire Desemba 19, 2024, alisababisha ajali eneo la Kisamba wilayani Magu, mkoani humo na kusababisha majeruhi kwa abiria 21. 

Alisema mshtakiwa huyo ambaye ni Mkazi wa National, jijini Mwanza alikuwa akiendesha gari kwa mwendokasi na bila umakini uliosababisha ajali na majeraha.

Alidai kitendo cha kusababisha majeraha hayo kwa abiria ni kinyume na sheria.

Dereva wa basi la Kisire linalofanya safari zake kati ya Mwanza na Sirari mkoani Mara, Adam Charles (30), akiongozwa na askari wa Jeshi la Polisi kuelekea katika Mahakama ya Wilaya ya Magu jana ambako alisomewa mashtaka 22 ikiwamo kusababisha majeruhi kwa abiria na uharibifu wa mali. PICHA: VITUS AUDAX
Hata hivyo mshtakiwa huyo alikana kutenda makosa hayo.

Mwendesha Mashtaka Nko alidai mahakamani kuwa upelelezi umekamilika na kuomba ipangwe tarehe nyingine kwa ajili ya kumsomea mshtakiwa maelezo ya awali na kupeleka mashahidi.

Baada ya hoja hizo, Hakimu Mkazi Mkuu wa mahakama hiyo, Erick Kimaro, aliruhusu dhamana kwa mshtakiwa akimtaka kuwa na wadhamini wawili wenye barua ya utambulisho wa Serikali ya Mtaa.

Pia, Hakimu Kimaro alisema wadhamini hao wanapaswa kusaini dhamana ya maneno ya Shilingi milioni tatu na kuwa na kitambulisho kinachotambulika.

Mshtakiwa alishindwa kukidhi masharti ya dhamana kutokana na kuwa na mdhamini mmoja pekee ambaye naye hakuwa na barua ya utambulisho iliyokidhi masharti hayo pamoja na kitambulisho.

Hakimu Kimaro aliahirisha shauri hilo hadi Januari 16, litakapoitwa kwa ajili ya mshtakiwa kusomewa maelezo ya awali ya shtaka linalomkabili.