Kwa mara ya kwanza katika historia, ndani ya treni ya SGR, umefanyika mjadala wa kusisimua wa kuchambua kitabu cha mwezi "The Diary of a CEO" pamoja na kuhamasisha umuhimu wa kujisomea vitabu hasa kwa vijana wa Kitanzania.
Tukio hilo la kipekee lilifanyika chini ya uongozi wa Hekima Book Club, kikundi cha vijana wanaohamasisha usomaji wa vitabu katika Mkoa wa Dar es Salaam na kuwa kivutio kwa abiria waliotumia usafiri huo.
Kiongozi wa Hekima Book Club Dar es Salaam, David James, alieleza, “Hekima Book Club kwa zaidi ya miaka minne sasa tumekuwa vinara wa kukuza tamaduni ya kujisomea. Lengo letu kuu ni kufanikisha kampeni hii kufika kila mkoa wa Tanzania, na hadi sasa tumefanikiwa katika mikoa mitatu – Dar es Salaam, Arusha, na Mwanza.” alisema
Aliongeza kuwa mjadala huo wa kitabu uliandaliwa kwa nia ya kuonyesha jinsi vitabu vinaweza kuwa daraja la maarifa, kujenga fikra chanya, na kuwahamasisha vijana kuchangamkia fursa za elimu. Washiriki wa mjadala huo walihamasishwa kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha usomaji wa vitabu unakuwa sehemu ya maisha yao ya kila siku.
Kwa miaka ya karibuni, utamaduni wa kujisomea vitabu nchini Tanzania umeanza kupata wafuasi wapya na kuonyesha dalili za ukuaji wa taratibu, ikiashiria nyota njema kwa siku zijazo.
David aliongeza kuwa, “Tumekuwa tukibuni mbinu mbalimbali ili kuona kampeni yetu inazaa matunda. Mojawapo ya mbinu hizi ni kukutana mwisho wa mwezi ambapo kila mmoja wetu atarudi nyumbani na kitabu kipya. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa katika kila nyumba hakukosi kitabu.”
Mjadala uliofanyika behewa namba 12 si tu ulikuwa wa kipekee, bali pia ulikuwa jukwaa la kuhamasisha vijana kutambua nafasi ya vitabu katika kuboresha maisha yao.
Hekima Book Club imeahidi kuendelea kuhamasisha na kupanua wigo wa kampeni yao hadi kufikia kila kona ya Tanzania.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED