Balozi Chen atoa kongole kwa TGL uandishi bora, kuimarisha uhusiano

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 06:16 PM Jan 07 2025
Naibu Meneja Mkuu wa The Guardian Ltd, Jackson Paulo akimkaribisha Balozi wa China nchini, Chen Mingjian, kutembelea kampuni hiyo jijini Dar es Salaam leo.
Picha: Miraji Msala
Naibu Meneja Mkuu wa The Guardian Ltd, Jackson Paulo akimkaribisha Balozi wa China nchini, Chen Mingjian, kutembelea kampuni hiyo jijini Dar es Salaam leo.

Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian ameipongeza Kampuni ya The Guardian Limited (TGL) kwa umahiri katika uandishi wa habari zenye maadili na ripoti zisizo na upendeleo.

Kauli hiyo ameitoa mapema leo wakati  wa ziara ya heshima katika makao makuu ya kampuni hiyo jijini Dar es Salaam yenye lengo la kujionea utendaji kazi na uandaaji wa gazeti.

Balozi Chen amesisitiza kuwa TGL imeweka viwango bora katika kutoa taarifa sahihi, za haki, na za uwiano, ambavyo ni muhimu kwa kukuza uelewa wa pande zote na kuendeleza maendeleo.

"The Guardian Limited imekuwa ikitoa taarifa za kitaalamu kuhusu uhusiano kati ya China na Tanzania pamoja na masuala ya kimataifa. Nawapongeza kwa mtazamo wenu usio na upendeleo na wa uwiano, ambao ni muhimu kwa kukuza uelewa wa pande zote na kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia kati ya mataifa yetu," amesema.

2. Balozi wa China akisalimiana na Meneja wa Teknolojia ya Habari, Allan Mshana.
Amebainisha kuwa hatua kubwa katika mkakati wa biashara wa China ilifikiwa mwaka jana wakati Rais Xi Jinping alipotangaza utekelezaji wa sera ya kuondoa ushuru kwa bidhaa muhimu zinazoagizwa kutoka nje. Balozi huyo pia amesisitiza uimara wa ushirikiano kati ya nchi hizi mbili, akitaja mauzo ya bidhaa za kilimo zenye ubora wa hali ya juu kama korosho na asali kutoka Tanzania kwenda China, pamoja na miradi mikubwa ya miundombinu kama Daraja la Magufuli na upanuzi wa Bandari ya Dar es Salaam.

Jackson Paulo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TGL, ametoa shukrani zake kwa balozi huyo na timu yake, akisisitiza umuhimu wa ushirikiano wao akiwahakikishia kuendeleza ushirikiano huo.

3. Mhariri Mtendaji wa gazeti Nipashe, Beatrice Bandawe, akitambulishwa kwa Balozi wa China nchini, Chen Mingjian.

"Tunashukuru sana Balozi na timu yake kwa kutembelea The Guardian Limited. Tunathamini sana hatua hii na tunatarajia ushirikiano wa siku za usoni katika moyo wa ushirikiano ambao utaendeleza uhusiano wetu," amesema.

Wallace Mauggo, Mhariri Mkuu wa The Guardian, amesifu mchango mkubwa wa China katika maendeleo ya miundombinu nchini Tanzania, akibainisha umuhimu wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) katika kuchochea ukuaji wa uchumi na kuboresha muunganisho kati ya nchi hizo mbili.

4. Balozi wa China akiangalia namna mchakato wa uchapaji wa magazeti unavyofanywa wakati alipotembelea kiwanda cha uchapaji cha The Guardian Ltd Mikocheni jijini Dar es Salaam mapema leo.

"Mchango mkubwa wa China katika maendeleo ya miundombinu umekuwa wa muhimu kwa maendeleo ya Tanzania, ambapo TAZARA inachukua nafasi kubwa kama chachu ya ukuaji wa uchumi. Ushirikiano huu wa kimkakati si tu unaboreshaji wa muunganisho wa kikanda bali pia unakuza biashara na harakati kati ya Tanzania na Zambia, jambo ambalo ni muhimu kwa ustawi wetu wa pamoja," amesema.