Vijana sita kizimbani kwa udanganyifu EFD, kusababisha hasara bilioni 2.1 kwa TRA

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 01:19 PM Jan 08 2025
Vijana sita kizimbani kwa udanganyifu EFD, kusababisha hasara bilioni 2.1 kwa TRA.
Picha:Grace Gurisha
Vijana sita kizimbani kwa udanganyifu EFD, kusababisha hasara bilioni 2.1 kwa TRA.

VIJANA sita wamefikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni, Dar es Salaam, wakikabiliwa na mashtaka 68, yakiwemo ya udanganyifu kwenye matumizi ya mashine za kielektroniki za EFD, na kuisababishia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) hasara ya Shilingi bilioni 2.1.

Vijana hao ni Stanslaus Mushi (27), mfanyabiashara na mkazi wa Malamba Mawili; Nemence Mushi (29); Rose Nanga (33), mhasibu wa soko na mkazi wa Kimara B; Hussein Mlezi (37), fundi wa kompyuta na mkazi wa Mbagala Kuu; Edwin Mark (22), mkazi wa Yombo Vituka; na Salim Salehe (45), mchoraji.

Mashtaka wanayokabiliwa nayo ni pamoja na kutumia mashine za EFD kwa njia zinazopotosha mfumo wa TRA, kuisababishia TRA hasara, na kupata usajili wa namba za utambulisho wa mlipakodi (TIN) na Ongezeko la Thamani (VAT) kwa njia ya udanganyifu.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Daisy Makakala, akisaidiana na Auni Chilamula, aliwasomea mashtaka hayo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Radhamani Rugemalira. Washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu mashtaka hayo kutokana na mamlaka ya mahakama hiyo kutokuwa ya kusikiliza kesi hiyo.

Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, katika shtaka la kwanza hadi la 64, washtakiwa wanadaiwa kuwa kati ya Novemba 1 na Novemba 30, 2024, walifanya udanganyifu katika mashine za EFD kwa lengo la kupotosha mfumo wa TRA, huku mashine hizo zikimilikiwa na Hadija Songea, na zikionesha kufanya mauzo pamoja na kutoa risiti mbalimbali za kughushi.

1

Shtaka la 65 na 66 linawakabili Mushi, Nanga, na Salehe, ambapo wanadaiwa kupata usajili wa namba za TIN kwa jina la Hadija Songea kwa njia ya udanganyifu, kosa linalodaiwa kufanyika kati ya Juni 1 na Juni 30, 2024.

Katika shtaka la 67, Mushi na Nanga wanatuhumiwa kusajili mashine za EFD kwa jina la Hadija Songea kwa njia ya udanganyifu, kosa ambalo linadaiwa kutendwa kati ya Juni 1 na Juni 30, 2024.

Shtaka la 68 linadai kuwa kati ya Novemba 1 na Novemba 30, 2024, ndani ya jiji la Dar es Salaam, washtakiwa waliisababishia TRA hasara ya Shilingi 2,160,310,567.51 kutokana na matumizi ya uongo ya mashine za EFD.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo, Hakimu Rugemalira aliwataarifu washtakiwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo, na hivyo hawakutakiwa kujibu lolote kuhusu mashtaka hayo. Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 20, 2025.