WAKATI akijipanga kuisaidia timu yake kutinga hatua ya robo fainali katika mashindano ya kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika, mshambuliaji wa Yanga, Clement Mzize, amesema anafurahi kuona jina lake linatajwa na klabu mbalimbali za nje ya Tanzania.
Mzize ambaye alionyesha kiwango kikubwa na kufunga mabao mawili katika ushindi wa magoli 3-1 dhidi ya TP Mazembe kutoka DR Congo, mechi iliyochezwa Januari 4, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, alisema anaamini muda ukifika kila kitu kitawekwa hadharani.
Mzize alisema anaamini bado mchango wake unahitajika kwa sasa ndani ya Yanga na akili yake yote ni kuona wanafanya vizuri katika mashindano ya kimataifa na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Nyota huyo alisema anajisikia furaha kubwa kuona wanaendelea Yanga inapata mwendelezo wa matokeo chanya katika kwenye mechi za kimataifa kwa sababu wanahitaji kufikia malengo ya kutinga hatua ya robo fainali ya michuano hiyo ya CAF (Shirikisho la Soka Afrika).
Aliongeza Mzize amesema kuwa walikuwa wanahitaji kupata ushindi kwenye mchezo wao dhidi ya TP Mazembe jambo ambalo liliwezekana licha ya ushindani kuwa mkubwa kwenye mchezo huo.
“Ilikuwa ni muhimu kwetu kupata matokeo mazuri licha ya ushindani ambao upo katika hatua hii, tunaamini tutazidi kupambana katika mechi zinazofuata ili tufikie malengo yetu, hakuna mechi rahisi katika hatua ya makundi, kila timu ina ubora,” alisema Mzize.
Tayari Al Hilal ya Sudan yenye pointi 10 tayari imeshatinga hatua ya robo fainali wakati MC Alger iko katika nafasi ya pili na pointi zake tano, mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga wanafuata wakiwa na pointi nne na TP Mazembe yenye pointi mbili inaburuza mkia.
Yanga imebakiza mechi moja nyumbani dhidi ya MC Alger kutoka Algeria na itasafiri kuifuata Al Hilal ambayo inacheza mechi zake mjini Lubumbashi, DR Congo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED