Chuo Kikuu cha Mzumbe kilichopo mkoani Morogoro kimewatoa hofu wanafunzi 1,636 ambao wana sifa ya kupata mikopo ya Serikali, baada ya baadhi ya taarifa kutangaza kuwa wamepewa muda wa ziada wa kujisajili hadi Januari 10 mwaka huu.
Hata hivyo, wanafunzi ambao hawapati mikopo hawakupewa muda wa ziada.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Morogoro leo, Makamu Mkuu wa Chuo, Profesa William Mwegoha, amesisitiza kuwa taarifa zilizozagaa kwenye mitandao ya kijamii siyo za kweli na zimekuwa zikipotosha wanafunzi, na kwamba chuo kitahakikisha kuwa wanafunzi wote wanajisajili.
Profesa Mwegoha amefafanua kuwa, kwa mujibu wa makubaliano na Menejimenti ya Chuo pamoja na Serikali ya Wanafunzi, wanafunzi wote wanapaswa kujisajili bila ubaguzi. Ameeleza kuwa barua iliyosainiwa na Naibu Makamu Mkuu wa Chuo tarehe 6 Januari mwaka huu ilikuwapo tafsiri tofauti ambazo sio sahihi.
Pia amefafanua kuwa, hadi sasa Chuo kipo kwenye wiki ya 10 ya masomo na tayari maandalizi ya mitihani yameanza. Amesema kwamba, baada ya tathmini, waligundua kuwa wanafunzi 1,636 hawajaisajili na walifanya makubaliano na Serikali ya Wanafunzi kuhusu jinsi ya kuhamasisha wanafunzi hao kujisajili.
"Kwa sasa, msimamo wa Chuo ni kuwa kila mwanafunzi anapaswa kujisajili bila kujali hali ya kifedha," amesema Profesa Mwegoha, akisisitiza kuwa hakuna mwanafunzi atakayekosa fursa kwa sababu ya changamoto za kifedha. Ameongeza kuwa chuo kimeamua kuchukua hatua dhidi ya aliyeandika barua iliyosababisha mkanganyiko huo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED