EACLC Ubungo yatakiwa kuwapa kipaumbele wafanyabiashara wazawa

By Pilly Kigome , Nipashe
Published at 06:20 PM Jan 09 2025
EACLC Ubungo yatakiwa kuwapa kipaumbele wafanyabiashara wazawa.
Picha: Mpigapicha Wetu
EACLC Ubungo yatakiwa kuwapa kipaumbele wafanyabiashara wazawa.

KITUO cha Biashara cha Kimataifa cha Afrika Mashariki na Kati (EACLC) kilichopo Ubungo, Dar es Salaam, kimetakiwa kuwapa kipaumbele wafanyabiashara wazawa kutoka Tanzania kwa kuwapatia maeneo ya kufanyia biashara.

Rai hiyo imetolewa Januari 7, 2024, na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dar es Salaam, Dk. Toba Nguvila, wakati wa ziara yake katika Halmashauri ya Wilaya ya Ubungo.

Akijibu agizo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa EACLC, Cathy Wang, raia wa China, amesema tayari wamelitekeleza na kufafanua kuwa hadi sasa asilimia 95 ya maduka yaliyochukuliwa yanamilikiwa na Watanzania.

Katika ziara hiyo, Dk. Nguvila pia alitembelea Kituo cha Afya cha Wilaya ya Ubungo na kuelezea kuridhishwa na maendeleo ya kituo hicho. Hata hivyo, alitoa maelekezo kwa uongozi wa hospitali hiyo kuanza ujenzi wa uzio kwa kutumia mapato yao ya ndani ili kuhakikisha usalama wa wagonjwa.

Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya cha Wilaya ya Ubungo, Dk. Nchang'wa Nhumba, alisema ujenzi wa kituo hicho ulianza Mei 2019 na huduma zilianza rasmi Desemba 2022. Ujenzi wake umekamilika kwa asilimia 99, na sasa wanakamilisha usakinishaji wa mashine za kuchomea taka.

Kwa sasa, kituo hicho kina uwezo wa kuhudumia wastani wa wagonjwa 6,000 hadi 7,800 kwa mwezi, ikilinganishwa na wagonjwa 1,000 hadi 1,200 waliokuwa wakihudumiwa awali. Wagonjwa wanaolazwa ni wastani wa 235 hadi 250 kwa mwezi. Dk. Nhumba aliongeza kuwa tangu huduma za mama na mtoto zianze kutolewa, vifo viwili pekee vimeripotiwa.

Aidha, Dk. Nguvila alikagua upanuzi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo na kubaini mapungufu kadhaa ndani na nje ya jengo hilo. Aliagiza watendaji husika kushughulikia changamoto hizo. Baadaye, alitembelea Soko la Mabibo kwa ukaguzi zaidi.