Raia wa Pakistan kizimbani kwa kusafirisha dawa za kulevya

By Imani Nathaniel , Nipashe
Published at 01:38 PM Jan 09 2025
Raia wanane wa Pakistan kizimbani kwa kusafirisha dawa za kulevya

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewapandisha kizimbani raia wanane wa Pakistan wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi kwa kusafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 22.52 na methamphetamine kilo 424.77.

Washitakiwa hao ni Mohamed Habifu (50), Mashaal Yusuph (46), Imtiaz Ahmed (45), Tayab Pettilwam (50), Immambakish Kudhabakish (55), Chand Mashaal (29), Akram Hassan (39), na Shehzal Hussein (45).

Mashtaka yao yamesomwa na Wakili wa Serikali, Titus Aron, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Beda Nyaki, baada ya kufikishwa mahakamani hapo leo.

Wakili Aron amedai kuwa Novemba 25, katika eneo la Navy Kigamboni, Dar es Salaam, washitakiwa wote walikutwa wakisafirisha dawa za kulevya aina ya heroine zenye uzito wa kilo 22.52 na methamphetamine kilo 424.77.

1

Baada ya kusomewa mashtaka yao, washitakiwa hawakutakiwa kujibu chochote kwa sababu shauri hilo ni la uhujumu uchumi na mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo.

Wakili Aron pia ameeleza kuwa upepelezi wa shauri hilo bado haujakamilika, na kuiomba mahakama kupanga tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo.

Hakimu Nyaki amebainisha kuwa, kutokana na kiasi cha dawa walizokutwa nazo, washitakiwa hao walikosa haki ya dhamana. Hivyo, wote wamerudishwa rumande.

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Januari 22, mwaka huu, kwa ajili ya kutajwa tena.