BoT yaonya matumizi ya fedha za kigeni ndani ya nchi

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 07:16 PM Jan 08 2025
Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba.
Picha: Mpigapicha Wetu
Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba.

Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeonya dhidi ya matumizi ya fedha za kigeni katika kufanya miamala ndani ya nchi, ikisisitiza kuwa kitendo hicho si tu kinahujumu uchumi wa nchi, bali pia ni kinyume cha sheria.

Hayo yamebainishwa leo Januari 8, 2025, jijini Dar es Salaam na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Emmanuel Tutuba, alipotoa taarifa kuhusu maamuzi ya Kamati ya Sera ya Fedha ya Benki Kuu kwa robo ya kwanza ya mwaka huu.

Gavana Tutuba amefafanua kuwa miamala yote inayofanyika ndani ya nchi inapaswa kufanywa kwa shilingi ya Kitanzania. Ameeleza kuwa matumizi ya sarafu za kigeni katika miamala ya ndani yanahujumu uchumi kwa sababu yanahusisha shughuli za uchumi wa Tanzania kwa kutumia sarafu za nchi nyingine, jambo ambalo ni kinyume cha sheria.

Akizungumzia maamuzi ya Kamati ya Sera ya Fedha, Gavana Tutuba amesema kuwa kikao hicho kimeamua kuendelea na kiwango cha Riba ya Benki Kuu (CBR) cha asilimia 6 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2025.

Uamuzi wa kutobadili kiwango hicho cha riba unalenga kuhakikisha kuwa uchumi unaendelea kuwa na ukwasi wa kutosha, kudhibiti mfumuko wa bei kubaki chini ya lengo la asilimia 5, na kuwezesha ukuaji wa kasi wa uchumi. Gavana amebainisha kuwa uchumi unatarajiwa kukua kwa kasi ya takriban asilimia 5.7 katika kipindi cha robo ya kwanza ya mwaka huu.