KAMATI ya Bunge ya Bajeti imesema hadi kufikia Juni, 2024 deni la Serikali lilikuwa Sh.Trilioni 96.8 sawa na ongezeko la asilimia 18.18 ikilinganishwa na Sh.Trilioni 81.9 katika kipindi kama hicho mwaka 2023.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oran Njeza ameyasema hayo leo bungeni alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za kamati hiyo.
Amesema ongezeko hilo lilitokana na ukopaji kwa ajili ya kugharamia miradi ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, reli, viwanja vya ndege, umeme na maji pamoja na kushuka kwa thamani ya Shilingi dhidi ya dola ya Marekani.
“Uchambuzi wa kamati ulibaini kuwa takribani asilimia 37.48 ya mapato ya ndani yaliyokusanywa katika mwaka 2023/24 yalitumika kulipa deni,”amesema.
Amesema Kamati inaendelea kuishauri Serikali kuhakikisha mikopo inayopokelewa inaelekezwa katika miradi inayochochea kasi ya ukuaji wa uchumi na mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi pamoja na kuongeza wigo na ukusanyaji wa mapato ya ndani ili kuwa na uwezo wa kugharamia deni.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED