Maisha ya watu, viumbe hatarini Ziwa Victoria

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:26 AM Feb 10 2025
Taka za plastiki zikiwa zimechanganyika na taka mbalimbali ndani ya Ziwa Victoria eneo la Nela, jijini Mwanza.
PICHA: MPIGAPICHA WETU
Taka za plastiki zikiwa zimechanganyika na taka mbalimbali ndani ya Ziwa Victoria eneo la Nela, jijini Mwanza.

USALAMA wa viumbe katika Ziwa Victoria na watumiaji wa rasilimali zake uko hatarini kutokana na taka za plastiki zinazoingia ziwani, wataalamu wakizitaja kuwa na athari za moja kwa moja kiafya na mfumo wa ikolojia.

Ziwa Victoria linatajwa kuwa chanzo muhimu cha maisha kwa zaidi ya watu milioni 40. Sasa limegeuka kuwa dampo lisilo rasmi la taka za plastiki, hata kuzua wasiwasi mkubwa kwa watumiaji wa maji na samaki kutoka ziwani huko.

Utafiti wa mwaka 2015 wa Jarida la Utafiti wa Maziwa Makuu uliofanyika mkoani Mwanza ukichunguza samaki sangara na sato wanaovuliwa Ziwa Victoria kwa njia za kienyeji, ulibaini kuwapo chembechembe za plastiki kwa asilimia 20 katika kila aina ya samaki wanaovuliwa ndani ya ziwa hilo. 

Hii ina maana kwamba samaki mmoja kati ya watano wanaovuliwa ziwani, alikutwa na chembechembe za plastiki.

Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004 (Kifungu cha 109) inaelekeza Mamlaka za Usimamizi wa Mazingira kulinda vyanzo vya maji dhidi ya uchafuzi, ikiwamo kuzuia taka za plastiki zinazoharibu mazingira.

Licha ya maelekezo hayo ya kisheria, uchunguzi wa mwandishi wa habari hii umebaini kuwa uchafuzi wa Ziwa Victoria unaosababishwa na taka za plastiki unaendelea kuongezeka.

"Taka ambazo mara nyingi hukutwa ziwani ni chupa za maji, chupa za soda, lakini pia kuna mifuko ya plastiki wanaita "vifungashio", hiyo ndiyo mingi zaidi," anaeleza Jerome Kayombo, Meneja wa Baraza la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Ziwa, katika mazungumzo maalum na mwandishi wa habari hii.

Kayombo anaeleza kuwa jiografia ya mkoa wa Mwanza inachangia Ziwa Victoria kupokea taka nyingi zinazotoka katika makazi ya watu, hasa wakati wa mvua. 

"Kimsingi kwa jinsi mkoa wa Mwanza ulivyo, Ziwa Victoria hupokea taka zote zinazobebwa na maji kutoka kwenye makazi ya watu. Kwa maana mvua ikinyesha, taka zote zilizopo kwenye maeneo ya watu zinapelekwa ziwani," anasema.

Hata hivyo, Kayombo anasema NEMC haijafanya utafiti wa kina kubaini kiwango halisi cha taka za plastiki ndani ya ziwa, lakini anakiri kusoma ripoti za taasisi zingine zinazoonesha ziwa hilo linakabiliwa na changamoto ya taka za plastiki. 

"Hatujafanya utafiti mkubwa wa kiwango hicho, wa kukaa na kujua hali ipoje, lakini ukisoma kwenye utafiti wa wenzetu, plastiki — hasa plastiki ndogo ndogo — ni changamoto kubwa sana ambayo inakuja kuukumba ulimwengu," anasema Kayombo.

Kitogo Lawrance, Ofisa Mazingira wa taasisi isiyo ya kiserikali ya EMEDO, anaeleza kuwa utafiti uliofanywa na taasisi hiyo miaka miwili iliyopita, ilibainika kuwapo ongezeko la taka za plastiki Ziwa Victoria, hasa katika maeneo ya Nyamagana, Ukerewe na Ilemela.

"Mwaka 2023, kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) pamoja na Shirika la Utafiti la Norway, tuligundua kuwa taka zilizoongoza katika uchafuzi wa Ziwa Victoria ni taka za plastiki. Hii inamaanisha vifungashio, chupa na vifaa vingine vyote vya plastiki," anaeleza Lawrance.

Taka za plastiki zikiwa zimechanganyika na taka mbalimbali ndani ya Ziwa Victoria eneo la Nela, jijini Mwanza.

"Ukiangalia hizo taka za plastiki katika maeneo hayo, unaona jinsi gani ziwa linavyochafuliwa," aliongeza Lawrance.

Ripoti ya Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP, 2021) inabainisha kuwa takribani tani 500 za plastiki huingia Ziwa Victoria kila mwaka, uchunguzi wa awali ukionesha taka hizo zinajumuisha mifuko ya vifungashio, chupa za maji ya kunywa, chupa za soda na makopo. 

Vilevile, Ripoti ya Ukaguzi wa Taka na Bidhaa (Waste and Branding Audits - WABA) iliyofanywa na shirika lisilo la kiserikali la Nipe Fagio mwaka 2020, inabainisha kuwa kati ya kilo 34,740 za taka zilizokusanywa katika mikoa 13 ya Tanzania, kilo 20,844 (sawa na asilimia 60) zilikuwa bidhaa za plastiki. 

Watafiti wa shirika hilo wanatafsiri takwimu hizo, wakisema ni hali inaonesha kiwango kikubwa cha matumizi ya bidhaa za plastiki katika jamii. Mvua ikinyesha, maji husomba taka hizo na hatimaye kuzimwaga ziwani.

"Taka hizi hubeba vitu tofauti, zikiwamo chupa za plastiki zilizotumika kuhifadhi kemikali za sumu, dawa za kuua wadudu au wanyama waharibifu. Baadhi ya chupa hizi huingia ziwani zikiwa na mabaki ya kemikali, hivyo kuhatarisha viumbe hai na shughuli nyingine za binadamu zinazotegemea maji ya ziwa," inasomeka sehemu ya ripoti hiyo.

Dk. Elias Nyanza kutoka Hospitali ya Rufani ya Kanda Bugando anasema plastiki ni hatari kwa watu wanaozitumia na wale wanaoishi katika mazingira yenye uchafuzi huo. 

"Madhara ni makubwa sana," anatoa tahadhari. "Taka hizi zinaathiri hali ya maji, zinaharibu mazalia ya samaki na zinaathiri mfumo mzima wa ikolojia wa Ziwa Victoria. Lakini kikubwa zaidi, plastiki hizi huingiza kemikali kwenye maji ambazo hazikuwapo awali."

Dk. Nyanza anaeleza kuwa taka za plastiki zinapoingia ziwani, huvunjika na kuwa vipande vidogo vidogo (microplastics) ambavyo ni hatari zaidi kwa viumbe wa majini, wakiwamo samaki. 

Anasema vipande hivyo vinaweza kuharibu mazalia ya samaki na kusababisha kupungua kwa idadi yao ziwani, jambo linaloweza kuwa na athari kubwa kwa watu wanaotegemea uvuvi kwa maisha yao. 

"Zikishavunjwa vipande vidogo, sumu zilizopo katika plastiki hizi huingia kwenye maji, huathiri samaki, mazalia yao na hatimaye viumbe hai wengine, wakiwamo binadamu wanaokula samaki hao," anaeleza Dk. Nyanza.

Kwa mujibu wa utafiti wa mwaka 2020 uliofanywa na Asasi ya AGENDA inayojihusisha na masuala ya mazingira na maendeleo, plastiki zina zaidi ya kemikali 500, zikiwamo zile zinazotumika kwenye viuatilifu, mafuta ya transfoma (PCBs), kemikali za viwandani na kemikali nyingine hatarishi.

Katika utafiti huo, sampuli moja ya plastiki ilikutwa na aina sita za kemikali hatari, zikiwamo kemikali za kuzuia moto kuwaka (brominated flame retardants), kemikali nne za kupunguza athari za mionzi ya jua (UV stabilizers) na moja aina ya Bisphenol A (BPA). Kemikali hizo huingia kwenye maji wakati taka za plastiki zinapooza na kuharibika ziwani.

"Ukija kuangalia samaki na mazao mengine ya ziwani, tayari yana mabaki ya sumu zitokanazo na plastiki," anafafanua Dk. Nyanza, ambaye pia ni Mhadhiri Mwandamizi katika Chuo cha Sayansi ya Tiba Bugando. 

"Shirika la Afya Duniani (WHO) limezitaja kemikali hizi kama sumu hatarishi, zinazosababisha madhara katika mfumo wa uzazi wa binadamu na zinaweza kuathiri ukuaji wa watoto wadogo, hasa vichanga," anafafanua.

Dk. Nyanza anaongeza kuwa baadhi ya kemikali zinazotokana na plastiki, zimetambuliwa kuwa na uhusiano na magonjwa kama saratani, lakini utafiti zaidi unahitajika ili kuelewa kiwango halisi cha athari zake kwa binadamu wanaotegemea Ziwa Victoria kwa maisha yao.

Anasema kuwa mbali na madhara hayo, mrundikano wa taka za plastiki katika maeneo mbalimbali pia husababisha harufu kali, hivyo kuathiri shughuli za kila siku hasa katika maeneo ya kando ya Ziwa Victoria. 

Irene John (37), mkazi wa mtaa wa Mswahili, jijini Mwanza, anasema: "Yaani hapa ukija asubuhi huwezi kuamini. Huwezi kupiga hatua mbili usikutane na taka za plastiki. Unaweza kukuta ni chupa ya soda, mifuko na chupa za pombe kali. Unajua hapa wavuvi wanatumia soda na mazingira ya hapa ni lazima tu utumie chupa za kutupa."

Irene anasema taka za plastiki zimezagaa maeneo ya ziwani, jambo ambalo hufanya maeneo ya fukwe ambazo shughuli za uvuvi hufanyika, kutokuwa na mvuto na hivyo kudorora kwa biashara katika maeneo hayo.

"Hata kama ni wewe, unakuja unakutana na chupa za plastiki ziko hapa zimejaa mkojo, zinatoa harufu, mara umeona mfuko wa plastiki una haja kubwa ya binadamu, hata kama ni wewe huwezi kuja tena hapa, utaona wale watu ni wachafu," analalama Irene akielezea hali halisi inayowakwaza wavuvi na wananchi wengine kwenye fukwe za Ziwa Victoria.

Abiud Samson (47), mvuvi na mkazi wa mtaa wa Kigoto wilayani Ilemela, jijini Mwanza, anasema chupa, mifuko na taka zinginezo za plastiki ni changamoto kubwa kwa wanaotegemea Ziwa Victoria kwa matumizi ya kila siku. 

Anaeleza kuwa yeye na familia yake wana hofu na afya zao kwa kuwa hulazimika kutumia maji ya ziwani kutokana na ukosefu wa maji safi kwenye maeneo wanakoishi.

Katika kujihami kwa nafasi yao, wanalazimika kuyachuja maji ya ziwa hilo mara kwa mara kabla ya kuyatumia.

*ITAENDELEA KESHO