KAMATI ya Bunge ya Bajeti, imesema kiwango cha uhimilivu cha Mfuko wa Pensheni kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ni asilimia 36.4 ikilinganishwa na kiwango kinachokubalika cha asilimia 60 na lengo la chini la uhimilivu la asilimia 40.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Oran Njeza ametoa kauli hiyo leo bungeni alipokuwa akiwasilisha taarifa ya mwaka ya shughuli za kamati hiyo.
Amefafanua kuwa mifuko ya Hifadhi ya Jamii imekuwa inafanya uwekezaji usio na tija ambapo kwa kipindi cha Mwaka wa Fedha 2021/22, 2022/23 Mfuko wa PSSSF umelipa mafao ya wastaafu yenye thamani ya Sh.Trilioni 4.34 na kupata faida ya Sh.Trilioni 1.8, hivyo takwimu zinaonyesha kiasi kilicholipwa ni kikubwa ukilinganisha na faida inayotokana na uwekezaji wake.
Amesema Bunge linaazimia kwamba Serikali ihakikishe kuwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii inasimamiwa ipasavyo katika kuhakikisha kuwa uwekezaji unaofanywa ni wa tija na unaendana na michango ili kupunguza vihatarishi na kuwezesha mifuko kulipa mafao ya wastaafu kwa wakati.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED