CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA, kimeweka bayana kiini cha mazungumzo yake na Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Warioba ofisini kwake leo jijini Dar es Salaam.
Mambo hayo ni kuhusu uchaguzi wa ndani ya chama uliomalizika hivi karibuni na pia kuhusu hali halisi kuhusiana na uchaguzi uliomalizika wa serikali za mitaa, vijiji na vitongoji wa mwaka 2024 na ulazima wa kuwa na mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi Tanzania ili kuwa na chaguzi zinazoaminika na zisizo na dosari.
Kwa mujibu wa taraifa iliyotolewa leo, Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Tundu Lissu aliongozana na Naibu Katibu Mkuu Bara, Amani Golugwa kumtembelea kiongozi huyo mstaafu.
Uchaguzi wa CHADEMA ulifanyika Januari 21, mwaka huu, na Lissu aliibuka mshindi huku aliyekuwa Mwenyekiti wa miaka 21, Freeman Mbowe akiangushwa.
Pia chama hicho kimetangaza msimamo kuwa hakitashiriki kwenye uchaguzi mkuu kama hakutakuwa na mabadiliko kwenye mifumo ya uchaguzi na kuwa na mazingira ya haki kwa wadau wote.
Aidha, kililalamikia uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27,2024 kwa wagombea wake wengi wa chama hicho kukatwa, watu wawili kufariki dunia na wengine kadhaa kujeruhiwa.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED